Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Conchesta Leonce Rwamlaza
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA (K.n.y. MHE. ROSE K. SUKUM) aliuliza:- Mpango wa Serikali kupeleka fedha za afya moja kwa moja kwenye Vituo vya kutolea huduma za Afya umesaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na stahiki za watumishi, lakini Waganga Wafawidhi hufanya kazi za Wahasibu na Maafisa Manunuzi na hivyo kusababisha kutotoa huduma kwa wagonjwa kwa wakati:- Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuajiri Wahasibu na Maafisa Manunuzi kwa kila Zahanati?
Supplementary Question 1
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu yake, anasema kwamba watumishi wanaweza kulipwa na Halmashauri lakini Halmashauri hizi hazina fedha. Kwa hiyo, nataka kujua kwa sababu Halmashauri hazina fedha Kifungu cha kuwalipa kitatoka wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matatizo ya Bima ya Afya kwa sababu kuna wakati mwingine Halmashauri zinashindwa kurejesha fedha katika Mfuko wa Bima, kwa hiyo, kunakuwa na matatizo ya upatikanaji wa dawa. Je, tatizo hili mtalimaliza namna gani? (Makofi)
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Mbunge anaulizia uwezekano uliopo wa Halmashauri kulipa. Kwanza utaratibu uliopo kama nilivyosema, ni kwamba manunuzi mengi ya dawa yanafanyika na wale Phamasists katika maeneo yetu ya wilaya. Ila kama Halmashauri ina uhitaji, huwa inaangalia pia na uwezo wake wa fedha; na kwa kawaida wanaomba kibali hapa TAMISEMI, tunawaruhusu wanaendelea kuwaajiri watu kwa mkataba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejibu kwenye swali langu la msingi kwamba kama Serikali itapata uwezo itawajiri wawe wa kudumu panapokuwa na mahitaji, kwa kuwa tayari shughuli kubwa ya manunuzi inafanywa na wataalam wenyewe kuangalia vizuri viwango na tunawasiliana na wenzetu wa MSD moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge alitaka kujua namna ambavyo kunakuwa na changamoto ya dawa katika maeneo haya. Hatujapata sehemu ambayo wameshindwa kununua madawa haya. Naomba tupokee hoja ya Mheshimiwa Mbunge tuifanyie kazi. Kama kuna Halmashauri imepata changamoto hii, basi tuwasiliane ili tupate namna ya kuitatua ili mradi wananchi wetu waendelee kupata huduma kama ambavyo Serikali imekusudia kuwapa huduma bora katika maeneo yao ya karibu. Ahsante.
Name
Maryam Salum Msabaha
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA (K.n.y. MHE. ROSE K. SUKUM) aliuliza:- Mpango wa Serikali kupeleka fedha za afya moja kwa moja kwenye Vituo vya kutolea huduma za Afya umesaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na stahiki za watumishi, lakini Waganga Wafawidhi hufanya kazi za Wahasibu na Maafisa Manunuzi na hivyo kusababisha kutotoa huduma kwa wagonjwa kwa wakati:- Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuajiri Wahasibu na Maafisa Manunuzi kwa kila Zahanati?
Supplementary Question 2
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa vyanzo vingi vya mapato vya Halmashauri vinaenda Mfuko Mkuu: Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha vyanzo vile vya Halmashauri vinarudi kwa wakati muafaka ili changamoto ambazo zinakabili Halmashauri zipate kutatuliwa?
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SRIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Juzi nilikuwa najibu swali hapa katika Bunge lako Tukufu ambalo liliuliza namna ambavyo Serikali imejipanga kuwezesha Halmashauri. Tukasema kwamba fedha hizi ambazo zimekusanywa kutoka maeneo ya Halmashauri yale, kuna Halmashauri kulingana na mapato yao walikuwa wanapata fedha nyingi zaidi kuliko Halmashauri nyingine na matokeo yake kuna baadhi ya maeneo mengi ya nchi yalikuwa hayawezi kupata miradi ya maendeleo hasa miradi ile mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejiandaa na imetoa maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kwamba ziko fedha ambazo zitasimamiwa na Hazina, tumewaambia wataalam wetu katika Halmashauri zetu waandae miradi ya kimkakati kama ni stendi au soko kadri watakavyoona wenyewe katika maeneo yao fursa ni ipi, wakiandika andiko linakuja TAMISEMI, linapitiwa na wataalam wa TAMISEMI, linapitiwa pia na wataalam pia wa Wizara ya Fedha kupitia Hazina na baadaye wanaridhia kuanzisha mradi huo mkubwa. Mradi huo ukianzishwa ukakamilika watakuwa watakura wanarejesha lakini pia watapata fedha ambayo ina uhakika, changamoto zingine zote katika maeneo yao zitamalizika kwa sababu wana fedha ya uhakika. Tunataka wakipata fedha hizo wapange miradi ya maendeleo ili waweze kuitekeleza kwa fedha ambazo wenyewe wanazisimamia na zinapatikana kwa wakati. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved