Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mary Deo Muro

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARY D. MURO (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENAN) aliuliza:- Je, ni lini Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) litajenga nyumba za bei nafuu ambazo wananchi wenye hali ya chini wataweza kununua?

Supplementary Question 1

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa shirika lilishajenga nyumba tayari na zimekosa wanunuaji, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba zile nyumba zinanunuliwa, itapunguza bei au itafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kujenga nyumba nyingi vile bila kuangalia mahitaji ya soko, je, Serikali haioni kama inapoteza hela za wavuja jasho? (Makofi)

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Muro kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimthibitishie kwamba hakuna nyumba zilizokosa soko mpaka muda huu. Nyumba zote ambazo zilijengwa kwa ajili ya kuuzwa baada ya kuona watu hawawezi kununua kwa kiasi kile ambacho tulitarajia, nyumba zote zile zimepangishwa na kama zipo ambazo hazijapangishwa ni chini ya asilimia mbili. Hiyo imetokana tu na namna ambavyo mahitaji yalivyokuwa yakiombwa awali kwa sababu maeneo mengi ambapo nyumba zilijengwa awali yalikuwa ni mahitaji ya halmashauri husika, waliomba kujengewa, lakini baadaye hawakuchukua. Kwa hiyo shirika limeamua kuzipangisha nyumba zile na sasa hivi zote zimepangishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lake la pili anazungumzia habari ya mahitaji ya soko. Mahitaji ya soko ya nyumba bado ni makubwa sana. Kwanza tukiangalia tunahitaji kuwa na nyumba walau milioni tatu ambazo tunatakiwa tujenge walau nyumba 200,000 kila mwaka, hatujaweza kufikia idadi hiyo. Kwa hiyo, bado mahitaji ni makubwa zaidi kuliko ambavyo tunatarajia na ndiyo maana sasa kuna nyumba za gharama nafuu zitaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali tukianza na hapa Makao Makuu ya nchi.

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. MARY D. MURO (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENAN) aliuliza:- Je, ni lini Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) litajenga nyumba za bei nafuu ambazo wananchi wenye hali ya chini wataweza kununua?

Supplementary Question 2

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makazi katika kushughulikia makazi, tunayo changamoto ya waajiriwa wapya, watumishi wapya na hasa wale wa kipato cha chini kumudu makazi bora hasa katika mazingira ambayo wamiliki wengi wa nyumba za kupangisha wanataka kodi ya miezi sita mpaka mwaka mzima jambo ambalo watumishi hawa hawawezi kumudu na hivyo kusababisha mazingira ya wao sasa kujihusisha na rushwa ili wapate fedha za kulipia kodi. Sasa Serikali haioni umefika wakati wa kuleta sheria itakayoharamisha kitendo cha wamiliki wa nyumba kudai kodi ya zaidi ya mwezi mmoja? (Makofi)

Name

William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Answer

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Nnauye, Mbunge wa Jimbo la Mtama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli jambo hili linaleta kero sana na kama Wizara tumeshalitolea maelekezo mara kadhaa kwa mujibu wa sera, Waziri wa Ardhi na Makazi ana uwezo wa kutoa maelekezo fulani fulani au kuweka kanuni zitakazoweza kutawala masuala haya yote yanayohusiana na makazi. Mimi nimeshawahi kutangaza na kupiga marufuku utaratibu huu kwa sababu sio wa kiungwana wala sio wa kisheria. Ni kweli kwamba watu wanalazimisha wapangaji kulipa miezi 12, si vijana wanaoanza kazi tu, hata wanafunzi wanaokaa kwenye hostel wanalazimishwa kulipa miezi 12, hili jambo halikubaliki hata kidogo. Serikali haitaingilia gharama ya upangishaji, upangishaji ni makubaliano ingawa iko katika utaratibu wa kuweka regulatory authority ambayo itaangalia na viwango vyenyewe vya upangishaji ili kulinda haki za wenye nyumba na haki za wapangaji vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili la kulazimisha mpangaji alipe miezi 12 au sita halikubaliki! Ila ni kweli kwamba ushauri wa ndugu Nnauye tunauchukulia maanani wakati tunasubiri Real Estate Regulatory Authority na sheria kuja Bungeni, tutaweka Kanuni kidogo itakayowabana hawa wasiosikia. (Makofi)

Name

John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. MARY D. MURO (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENAN) aliuliza:- Je, ni lini Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) litajenga nyumba za bei nafuu ambazo wananchi wenye hali ya chini wataweza kununua?

Supplementary Question 3

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika swali la msingi iliulizwa kuhusu Shirika la Nyumba la Taifa na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu. Katika Jimbo la Kibamba, Shirika la Nyumba la Taifa lilikabidhiwa eneo kubwa kidogo kwa ajili ya ujenzi wa Mji wa Viungani wa Luguruni kwa maana ya Luguruni Satellite Town ambayo ingehusisha nyumba za gharama nafuu, nyumba za kupangishwa, nyumba za kibiashara na miundombinu mingine. Hata hivyo, kwa miaka mingi pamoja na National Housing kupewa jukumu la kuwa mwendelezaji mkuu mpaka sasa hakuna chochote kilichoendelea na kimsingi eneo lile limeanza kugeuka kuwa kijipori.

Je, ni lini hasa National Housing itatekeleza huu wajibu wa kwenda kuujenga Mji wa Luguruni ikiwemo ujenzi wa nyumba za gharama nafuu?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnyika kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli National Housing wana eneo kule Luguruni na walikuwa wamepanga kujenga Satellite City kama ambavyo mkakati ulivyokuwa umepangwa. Eneo hilo halijajengwa mpaka sasa si kwamba limetelekezwa, isipokuwa katika ujenzi, bado kuna utaratibu ambao unaendelea katika kuhakikisha kwamba miradi yote ambayo ilikuwa inasimamiwa na imepangwa kujengwa, inajengwa. Kwa hiyo eneo lile mpaka sasa taratibu ziko vile vile na tungependa kutoa rai watu wasivamie eneo kwa sababu bado matumizi yapo pale pale kama ilivyopangwa. Nami nimhakikishie tu baada ya hii miradi mingine inayoendelea kukamilika, mji ule utajengwa kama ilivyokuwa imepangwa.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongeze kidogo kwamba maeneo mengi ambayo yamechukuliwa na National Housing nchi hii, mengine tumeweka kama Land Bank ya Serikali kwa sababu National Housing ndiyo mwendelezaji mkuu wa miliki kuliko waendelezaji wengine. Sisi tulijua lile eneo tusingelichukua sisi leo lisingekuwepo na ndiyo maana kwa sababu tumelichukua sisi hakuchukua mtu binafsi, tumeweza kuwapa hawa Ubungo eneo la kujenga wilaya pale Luguruni hivi sasa. Tumeweza kuwapa watu wa MSD kujenga ghala kubwa, walikuwa wanatumia zaidi ya bilioni tatu kupanga kwa ajili ya kuweka dawa lakini tumeweza kuwapa pale. Kwa hiyo wasichukulie tu kwamba maeneo tunayachukua National Housing ni kwa ajili ya uendelezaji wa haraka, lakini tuliya-protect kutokana na manyang’au wanaotaka kulangua ardhi zote za msingi katika maeneo ya miji na kuweka Land Bank.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kwa taarifa yake Mheshimiwa nataka nimhakikishie kama isingekuwa National Housing kuchukua lile eneo wao wasingepata mahali pa kujenga Makao Makuu ya Wilaya.

Name

Susan Anselm Jerome Lyimo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARY D. MURO (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENAN) aliuliza:- Je, ni lini Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) litajenga nyumba za bei nafuu ambazo wananchi wenye hali ya chini wataweza kununua?

Supplementary Question 4

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri ni kweli kwamba kwa Jiji la Dar es Salaam tunajua kwamba population ni kubwa sana lakini National Housing wamechukua maeneo na hasa eneo la Kawe ambalo ni Satellite City na walishaanza ujenzi pamoja na pale Morocco Square. Nataka kujua, ni kwa nini ujenzi huo umesimama na ni lini wataendeleza ili wananchi wa Dar es Salaam waweze kupata makazi salama? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Susan Lyimo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli miradi ile ilianza na ikawa imesimama na ilisimama tu sio pengine kwamba National Housing wameshindwa kuendeleza, lakini kulikuwa na taratibu za kisheria ambazo zilikuwa zinafuatwa ili kuweza kukamilisha. Napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kuanzia sasa ataona miradi ile inaendelea tukianza na Morocco Square kwa kutumia mapato ya ndani ya National Housing wanakwenda kujenga majengo yale na kukamilisha, kwa hiyo hatutakuwa na viporo tena. Tunamaliza Morocco Square then tunaenda kule seven eleven ya Kawe. Hayo yote yako kwenye Mpango na Bodi mpya ambayo inafanya kazi hiyo imeweka Mpango Kazi wa kuhakikisha miradi viporo yote ya National Housing inakamilika kutokana na schedule walivyojipangia. Kwa hiyo niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge, miradi hiyo yote inakwenda kuanza kukamilishwa.