Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO (K.n.y. MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI) aliuliza:- Ubunifu wa kupata ajira ni miongoni mwa changamoto kubwa kwa vijana hapa nchini:- Je, ni lini Serikali itabuni na kusimamia mkakati wa kuwajengea uwezo wa kujiajiri vijana kuanzia shule za msingi?

Supplementary Question 1

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri lakini pamoja na pongezi hizi naomba niulize maswali madogo mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni mkakati gani ambao umewekwa na Serikali wa kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kujiajiri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tumekuwa tukishuhudia vijana wengi wanajishughulisha na shughuli za kilimo. Je, Serikali haioni kwamba iko haja sasa ya kuona wale vijana ambao wanajishughulisha na shughuli za kilimo waweze kupata mafunzo na kwa kuwa tunafahamu kilimo ni uti wa mgongo ili waweze kufanya kazi zao kwa umakini na waweze kupata tija? Ahsate.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Sikudhani Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anafuatilia masuala ya vijana na akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la mkakati, ni kweli kwa kutambua kwamba ujasiriamali hivi sasa ni nguzo muhimu ya kumfanya kijana aweze kujiajiri, hivi sasa tumeshatambulisha mtaala wa ujasiriamali kuanzia ngazi ya chini mpaka elimu ya vyuo vikuu. Pia mkakati wa Serikali hivi sasa ni kuendelea kuwapitia wajasiriamali wote nchi nzima kwa kuwapa mafunzo katika kila Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, navyozungumza hivi sasa tumeshakamilisha mikoa zaidi ya 14 katika awamu ya kwanza na tutakwenda kumalizia awamu ya pili ambapo kila mkoa tumekutana na wajasiriamali zaidi ya 500 katika kuwapa elimu na ujuzi wa namna ya kuweza kufanya biashara zao.

Kwa hiyo, Serikali inatambua umuhimu huo wa wajasiriamali na ndiyo maana katika moja ya mkakati wetu ni kuwapa elimu na kuwasaidia pia kuweza kupata mikopo ya masharti nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu vijana kushiriki kwenye kilimo, Ofisi ya Waziri kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo tunao mkakati maalum wa kuwahusisha vijana katika kilimo ambao tumeanza kuutekeleza. Navyozungumza hivi sasa tunayo programu ya kilimo cha kitalu nyumba ambacho kitawafikia vijana 18,800 nchi nzima ambako kila Halmashauri nchi nzima vijana 100 watafundishwa kuhusu kilimo cha kitalu nyumba na vijana 20 watapata ujuzi wa kuweza kufundishwa kutengeneza green house. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba vijana wengi wa Kitanzania wanashiriki moja kwa moja katika uchumi wa viwanda kupitia sekta hii ya kilimo. Lengo letu ni kuwafikia vijana 47,000 katika mwaka huu wa fedha.