Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Emmanuel Adamson Mwakasaka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Primary Question
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya madeni mbalimbali ya wazabuni wanaoidai Serikali:- Je, Serikali imefikia hatua zipi katika kuhakikisha inalipa madeni ya wazabuni nchini?
Supplementary Question 1
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wazabuni wengi na nina imani hii ni kwa nchi nzima lakini hapa niwe specific kwa Tabora, ni wafanyabiashara wadogowadogo na wengi wapo sokoni wamekuwa waki-supply vyakula mbalimbali Serikalini kwa maana ya magereza na hata shuleni. Wengi wa wazabuni hao pamoja na kuhakikiwa madeni yao, hawajalipwa kuanzia mwaka 2013, inafika miaka sita (6) sasa na wazabuni hawa wengi wamekopa kwenye mabenki. Leo hii wengine wameuziwa nyumba zao na wengine wana kesi mbalimbali mahakamani. Serikali inasemaje kuhusu suala hili la kuwalipa wazabuni hawa kwa sababu madeni yao ni ya muda mrefu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwa na mtindo wa walipaji ambao wapo kwenye malipo mbalimbali hayo ya wazabuni kulipa madeni ya karibuni yaani wao kwa mfano deni ni la mwaka huu au la mwaka jana wanalipa hayo kwanza, yale ya miaka mingi ambayo watu wamekuwa na madeni haya ambayo yamepelekea mpaka kuuza nyumba zao hawalipi. Serikali inasemaje kuhusu hilo suala hilo? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwakasaka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza kwamba wapo wazabuni tangu 2013 hawajalipwa. Naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu kama nilivyosema kwenye jibu la msingi imekuwa ikilipa madeni haya kila mwaka. Kuanzia mwaka 2016/2017 tulitenga bajeti ya shilingi bilioni 625 na tukalipa shilingi bilioni 746. Mwaka 2017/2018 tulitenga shilingi trilioni 1 kwa ajili ya ulipaji wa madeni na tukalipa shilingi trilioni 1.096. Mwaka 2018/2019 tumetenga shilingi bilioni 600 na tukalipa shilingi bilioni 600.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumeendelea kulipa madeni haya. Sasa linalonishangaza ni kusema kuna wazabuni wadogowadogo wa tangu mwaka 2013. Naomba nitoe wito wangu kwa Makatibu Tawala wa Mikoa wote waweze kuwasiliana na wazabuni kwenye mikoa yao ili wahakikishe kama madeni yao bado ni halali kwa sababu madeni yote ambayo ni halali tumekuwa tukiyalipa mpaka mwaka 2020/2021 tutakuwa tumekamilisha kulipa madeni yote na deni lililopo sasa ni shilingi bilioni 325 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili ni kwa nini wanalipa madeni ya karibuni. Tuna vigezo vya ulipaji wa madeni haya, kigezo kimojawapo ni kuhakikisha kuwa madeni ya zamani yanapewa kipaumbele kwenye kulipwa. Kwa hiyo, nitoe wito wangu kwa Maafisa Masuuli wote wanapopelekewa fedha za kulipa madeni wafuate vigezo walivyopewa na Mlipaji Mkuu wa Serikali ili tuweze kuwasaidia wazabuni wetu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved