Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Dalaly Peter Kafumu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igunga
Primary Question
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:- Asilimia 70 au zaidi ya maeneo ya Kata za Isakamaliwa, Mbutu, Igunga, Nguvumoja, Lugubu na Itumba katika Jimbo la Igunga na Kata za Igoweko katika Jimbo la Manonga yapo ndani ya Mbuga ya Wembere ambayo kwa sasa imekosa sifa ya kuwa hifadhi ya wanyama na wananchi katika Kata hizo wameongezeka na kufanya kukosekana kwa maeneo ya makazi, kilimo na ufugaji na kwa kutokuwepo mipango mizuri ya matumizi bora ya ardhi kwa sababu ya hifadhi hiyo na kusababisha migogoro mikubwa kati ya wakulima na wafugaji na kuleta mauaji:- Je, ni lini Serikali italitenga na kulipima eneo la Hifadhi ya Wembere hususan katika maeneo ya Kata hizo kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, napenda nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake nina maswali mawili ya nyongeza;
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye swali la msingi Kata za Isakamaliwa Mbutu, Igunga, Nguvumoja, Lugubu, Itumba na Igoweko kwenye Wilaya ya Igunga zimo ndani ya Mbuga ya Wembere na mimi nilizaliwa na kukulia humo na kuna migogoro mikubwa sana ya wafungaji wakulima pamoja na mbuga hiyo.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni kwa nini ile Kamati ya Mawaziri iliyokuwa imeagizwa na Mheshimiwa Rais kupitia maeneo ya namna hii ili kutafuta suluhisho haikufika Igunga?
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni lini Serikali itapima eneo hili kupunguza maeneo ambayo yamekosa sifa kuwapa wananchi, lakini maeneo ambayo yanahitaji kuhifadhi kama alivyoeleza umuhimu wake yaendelee kutumika?
Name
Constantine John Kanyasu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia kwa umakini sana utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais kuhusu maeneo yote yenye migogoro na ambayo wananchi tayari wamekwishaanza kuyatumia lakini yamepoteza hadhi ya kuifadhi. Kwa ujumla wake pamoja na Wabunge wengine taarifa hii kama nilivyojibu kwenye Swali la Mheshimiwa Mipata iko mezani kwa Mheshimiwa Rais na tunasubiri maelekezo.
Mheshimiwa Spika, kwa kujibu swali lake la kwanza Kamati ilipewa mwezi mmoja kuwa imekamilisha taarifa ya nchi nzima na kwa kweli haikuweza kuzunguka nchi nzima kufikia maeneo yote, lakini kwa kutumia mfumo wa Serikali ambayo ipo kila sehemu kupitia Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, Kamati ilipokea maeneo yote yenye malalamiko ya nchi nzima. Kwa hiyo, ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba eneo hili pamoja na Kamati kutokufika katika eneo hilo, limo ndani ya mjadala ambao tuliuendesha katika Kamati ya Mawaziri Nane na majibu yatakapotoka itakuwa pamoja na eneo hili.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni lini Serikali itaondoa maeneo ambayo yamepoteza hadhi ya uhifadhi. Yapo maeneo mengi nchi nzima yenye hali kama hii na ndiyo ambayo sasa hivi yamevamiwa na wananchi na tumeelekezwa na Serikali kuangalia kama yamepoteza hadhi tupendekeze kuyaachia ili wananchi waweze kuyatumia, pamoja na swali lake la kwanza tunasubii maelekezo ya Kamati ambayo Mheshimiwa Rais aliiunda.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Kafumu ambaye katika nyakati tofauti tofauti amewaleta wazee kutoka katika Kata zilizoathirika nami binafsi nimeonana nao na kuwapa ahadi kwamba maombi yao yamefika mahala muafaka na tutayashughulikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili kuongezea kwenye majibu mazuri aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba katika mchakato wa kuchora ramani upya ya Pori Tengefu la Wembere ili kulipandisha hadhi sehemu yake kuwa Pori la Akiba tutazingatia maombi ya wananchi wa Kata ambazo zimetajwa, eneo la pori la akiba litakalobaki litakuwa dogo zaidi kuliko hili la square kilometa zaidi 8,000 lililopo sasa. Lengo hasa ni kubakisha walau eneo dogo ambalo litakuwa intact na ambalo tutalilinda ipasavyo kwa ajili ya faida za kiuhifadhi na hiyo connectivity kati ya hifadhi zilizopo kusini na hifadhi ambazo ziko upande wa Kaskazini, maombi ya wananchi yatazingatiwa na kwa hivyo eneo ambalo wanaweza kulitumia kwa kufuga kwa kilimo na kwa makazi litabaki kwa wananchi na wataishi kwa uhalali kuliko ilivyo sasa wananyanyasika.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved