Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Anna Richard Lupembe
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Primary Question
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu wa Sayansi katika Mkoa wa Katavi?
Supplementary Question 1
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mahitaji ya walimu wa sayansi ni makubwa sana na ukizingatia wananchi ambao tunaishi pembezoni unakuta shule moja kama Rungwa Sekondari pale Mpanda ina watoto 1,150, walimu wa sayansi kuanzia Form One mpaka Form Six walimu wako wanne tu. Na ukiangalia sehemu nyingine kama Usevia shule Form One mpaka Form Six walimu wawili.
Je, Serikali itatuletea lini Mkoa wa Katavi walimu kwa sababu tunahitaji sana walimu kutokana na uhitaji wa wanafunzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili,kwa kuwa Serikali ilifanya kazi kubwa ya kuhamasisha kujenga maabara katika shule zote za Kata nchini, na wananchi walihamasika sana wakajenga maabara na maabara zile zimekamilika lakini walimu wa sayansi hakuna kabisa.
Je, lini Serikali itaweka mikakati maalum kama ilivyofanya kuhamasisha kujenga maabara ili tuweze kupata sasa walimu wa sayansi? (Makofi)
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza ninampongezasana Mheshimiwa Mbunge Anna Lupembe kwa kuendelea kuwasemea watu wake wa Mkoa wa Katavi ili waweze kupata elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tuna changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi na hasa katika masomo ya sayansi na hisabati. Vilevile Serikali imefanya kazi kubwa sana ya kuongeza juhudi ya kutafuta fedha ili tuweze kuajiri walimu hawa wakasaidie kuondoa changamoto ya walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwataarifa tu mwezi Mei mwaka huu Serikali ilipeleka fedha za EP4R motisha ili moja, zikamalizie maboma ya shule za msingi na sekondari, pili ilikuwa ni ku-balance ikama katika shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaelekeze Waheshimiwa Wakurugenzi katika Halmashauri zetu na Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya, zile fedha za Serikali ilikuwa ni kuangalia kama kuna shule moja ina upungufu, shule nyingine ina walimu wa ziada, ilikuwa ni kuwahamisha kutoka eneo moja kwenda lingine ili kuweza ku-balance Ikama na kupunguza changamoto ya Walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kama nilivyosema katika maswali yaliyopita leo asubuhi, tumeshaomba kibali cha kuajiri walimu hawa, zaidi ya 15,000. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na maeneo mengine ya pembezoni, tutakapopata kibali cha kuajiri walimu wa sayansi na hisabati, maeneo ya pembezoni yatakuwa kipaumbele, tutaanza na maeneo ambayo yana upungufu mkubwa wa walimu kwenda pale ambapo pana upungufu ambao siyo mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anaulizia maboma ya maabara zetu. Ni kweli, tumekubaliana tunagawana kazi, Waheshimiwa Wabunge, Serikali na wadau mbalimbali wa elimu na maendeleo.Kazi ya kumalizia maboma haya ya maabara ni ya kwetu sote kama nilivyotaja. Serikali tumejipanga, hapa tulipo tupo kwenye manunuzi, wakati wowote kuanzia sasa taratibu za manunuzi zitakamilika tutapeleka vifaa katika maabara zetu. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na wadau wengine tuendelee kuchangia kwa namna mbalimbali tumalizie maboma yetu, vifaa tutapeleka, wataalam tutapeleka na hii changamoto hatimaye itaisha ili watoto wetu waweze kusoma katika mazingira ambayo ni rafiki. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved