Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Issaay Zacharia Paulo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Primary Question
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY Aliuliza:- Katika mradi wa REA I na II vijiji vingi vya Jimbo la Mbulu Mjini havikufikiwa na umeme na katika vijiji vilivyofikiwa ni kaya kati ya 20 mpaka 30 pekee ndizo zilizopata umeme:- (a) Je, ni lini REA III itapeleka umeme katika Vijiji 26 vya Jimbo la Mbulu Mjini? (b) Awamu ya I na II ziliruka shule nyingi, vituo vya afya na Makanisa. Je, ni lini sasa taasisi hizo zitapelekewa umeme? (c) Je, ni lini Serikali itarudia usambazaji wa umeme katika vijiji vyote vilivyosambaziwa sehemu ndogo sana katika Jimbo la Mbulu Mjini?
Supplementary Question 1
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu na Serikali nzima, Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote kwa kazi kubwa wanayofanya katika nchi yetu hususani Jimbo la Mbulu Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu madogo ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa mahitaji ya umeme katika Jimbo la Mbulu Mji ni makubwa; na kwa kuwa Jimbo la Mbulu Mji sehemu nyingi zilikosa umeme wakati wa REA I na II. Je, sasa Serikali inachukua hatua gani kwa wale wananchi ambao hadi sasa wameendelea kuachwa na umeme umeshapita kwenye maeneo yao na maombi yao hayajibiwi na Ofisi yangu ina orodha kubwa sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mahitaji ni makubwa sana ya chombo kinachoitwa UMETA (Umeme Tayari) na kwa kuwa majengo mengi katika Jimbo la Mbulu Mjini yako mbalimbali kwa maana ya nyumba za wananchi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta chombo hiki cha UMETA kwa kiasi kikubwa ili kuwapatia wananchi umeme ambao wana uhitaji mkubwa sana?
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini. Nampongeza kwa kazi nzuri anayoifanya katika Jimbo lake hususani katika kufuatilia sekta ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ameuliza Serikali ina mpango gani kwa kuwa mahitaji ya umeme ni makubwa na kwa maeneo mbalimbali ambayo hayajafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia Serikali yetu kuna Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B ambapo Mkoa wa Manyara ni miongoni mwa mikoa 16 ambayo itahudumiwa. Kwa sasa Mshauri Elekezi Multiconsult na Norplan wanaendelea kuhakiki vitongoji katika maeneo mbalimbali. Mradi huu utafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa kwa Euro milioni 100 na unatarajiwa kuanza mapema mwakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sambamba na miradi ya REA III ambayo itaendelea kupitia TANESCO, nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada hizi na huu Mradi wa Ujazilizi kwenye maeneo ambayo umepita vitongoji vimeachwa, Jimbo lake la Mbulu Mjini nalo litazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameulizia masuala ya kifaa kinachoitwa UMETA. Kwanza Serikali kupitia utekelezaji wa Mradi wa REA III, Mzunguko wa Kwanza vimetoa UMETA 250 kwa kila mkandarasi ambapo vinagaiwa bure kwa makundi maalum. Sambamba na hilo, kwa kuwa tumeona uhitaji ni mkubwa Shirika la TANESCO na REA wanaendelea na mchakato wa kuhakikisha UMETA inapatikana kwa bei nafuu ambayo ni Sh.36,000 ambapo kila mwananchi ana uwezo wa kumudu.
Kwa hiyo, niendelee kutoa maelekezo kwa niaba ya Waziri wa Nishati, TANESCO na REA kuendelea kusambaza UMETA hasa kwenye taasisi za umma ambazo hazina mahitaji makubwa na wananchi wa kawaida. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved