Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE Aliuliza:- Idadi ya watu nchini inaongezeka kwa kasi sana na watu wanahitaji maendeleo; aidha ukuaji huu una matokeo hasi na chanya:- Je, Serikali ina mikakati gani ya kutumia au kudhibiti kasi ya idadi ya watu?
Supplementary Question 1
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Amejieleza vizuri, tumeyaona kwenye karatasi hapo na yapo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya watu katika nchi yetu inaongezeka na toka tumepata uhuru mwaka 1961 na Muungano 1964 tumeendelea kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini. Angalau haya mawili ya maradhi na ujinga tunaelekea kuyamudu ndiyo maana idadi ya watu inaongezeka.
MWENYEKITI: Swali, swali!
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali; Serikali ina mpango gani sasa wa kupambana na adui namba moja ambaye ni umasikini unaoongezeka katika maeneo mengi hasa maeneo ya vijijini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kumekuwa na makundi makubwa ya vijana wanaohitimu elimu hasa Elimu ya Vyuo Vikuu. Sasa ndhi yetu ipo kwenye mkakati wa kujenga viwanda: Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwekeza katika viwanda vya Labor Intensive badala ya Capital Intensive ili kukidhi makundi makubwa ya vijana yanayohitimu shule na kwa sababu fursa tunazo? (Makofi)
Name
Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba umasikini ndani ya nchi yetu hauongezeki, unapungua kila mwaka. Hii naisema, siyo maneno yangu, ni maneno ya utafiti ambao umefanyika. Utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi uliofanyika mwaka 2018 na Mheshimiwa Waziri Mkuu akauzindua utafiti huu, unaonesha kwamba umasikini wa kipato umepungua kutoka asilimia 28.2 toka mwaka 2012 na sasa umefika asilimia 26.8 mwaka 2018. Hivyo siyo sahihi kuendelea kuimba wimbo wa Taifa letu kwamba watu wanazidi kuwa masikini. Siyo sahihi hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti huu pia unaonesha umasikini wa chakula kwa Watanzania katika kila kaya, mwaka 2012 ulikuwa asilimia 9.7; mwaka 2018 umasikini wa chakula kwa kaya ya kila Mtanzania ni asilimia 4.4. Kwa hiyo, tunaomba Watanzania wafahamu kwamba jitihada za Serikali yao na wao Watanzanzia wamejitolea kuelewa jitihada hizi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake wanafanya kazi kwa jitihada zote. Umasikini wa kipato na umasikini wa chakula umepungua kutokana na tafiti zilizofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili kwamba tuwekeze kwenye viwanda ambavyo vinatumia rasilimali watu zaidi kuliko kutumia capital intensive. Naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba katika viwanda ambavyo vimeanzishwa na vinaendelea kujengwa kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri wa uwekezaji asubuhi, ni viwanda vinavyotumia zaidi rasilimali watu. Viwanda hivi ni vile ambavyo vipo katika maeneo ya nguo. Tunafahamu hatujafanya vizuri zaidi, lakini jitihada zinaendelea kufanyika. Viwanda vya kutengeneza tiles havitumii mashine, vinatumia rasilimali watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vingine ni vya kuchakata mazao yetu, havitumii capital, vinatumia zaidi rasilimali watu. Nawaomba Watanzania wanaomaliza Vyuo Vikuu waweze kwenda kufanya kazi kwa tija kwenye viwanda hivyo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved