Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANATHROPIA L. THEONEST (K.n.y. MHE. GIMBI D. MASABA) Aliuliza: Wilaya mpya ya Itilima haina Mahakama ya Wilaya, jambo linalosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi kwenda Wilaya jirani ya Bariadi kupata huduma hiyo:- Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya Itilima?

Supplementary Question 1

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya Serikali kuahidi kwamba inaenda kujenga jengo hilo la Mahakama ya Wilaya katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020, bado Mahakama ya Bariadi inapitia changamoto ya upungufu wa Mahakimu, hivyo kusababisha kesi nyingi kuchelewa: Je, Serikali ina mpango gani kwa wakati huu mfupi kuisaidia Mahakama ya Bariadi ili iweze kukidhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wakati wananchi wa Itilima wanatembea kilometa 37, wenzao wa Wilaya ya Kyerwa wanatembea zaidi ya kilometa 100. Wananchi wa Murongo, Kaisho, Bugomora, Bugara, wanatembea umbali mrefu kufuata hiyo huduma katika Mahakama iliyoko Wilaya ya jiraniā€¦

MWENYEKITI: Swali! Uliza swali!

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali. Ni mkakati gani wa muda mfupi kuwasaidia wananchi wa Kyerwa waweze kupata huduma katika wilaya yao kabla ya kufikia mwaka 2019/2020. Nakushukuru. (Makofi)

Name

Dr. Augustine Philip Mahiga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Bariadi inafanya kazi nzuri sana. Hivi karibuni nilipitia kule na nikaona msongamano wa kesi mbalimbali. Ni moja ya majukumu makubwa ya Wizara hii, siyo tu kujenga Mahakama katika ngazi mbalimbali, lakini kutoa mafunzo kwa Mahakimu kadri ujenzi unavyoendelea. Hii inaenda sambamba na kuwasaidia wananchi kwa kuwapa haki ya kusimamia mashauri yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili. Mahakama ya Wilaya ya Kyerwa inahitaji kupata Mahakama yake mara moja. Katika mpango wa Mahakama ya Tanzania kama nilivyoeleza siyo tu tunataka kuleta Mahakama karibu na wananchi, lakini kuhakikisha kwamba tunapunguza kero ambazo wananchi wanapata ili kupata haki yao na kwa wakati. Kutokana na mkakati huo, tutaendelea kusomesha Mahakimu katika ngazi mbalimbali na tutaendelea kupanua ujenzi wa Mahakama katika ngazi mbalimbali hasa katika wilaya hiyo ambayo Mheshimiwa umeizungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.