Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Kasheku Musukuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Primary Question
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:- Je, ni kwa nini mgodi wa GGM umegoma kulipa deni la Halmashauri ya Geita la Dola za Kimarekani 800,000?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nashukuru pia majibu ya Serikali lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mji na Geita Vijijini, tulikuwa tunaudai Mgodi wa Geita kiasi cha dola 12,830,000 na anafahamu vizuri kwamba ilifikia mahali mpaka tukaandamana tukawekwa ndani mimi nikiwa mmoja wao. Baada ya kutolewa pale tulikaa kwenye kikao cha pamoja pamoja na Wizara ya Madini na TAMISEMI, Waziri akaamua kwamba wakatulipe kwanza dola 800,000 halafu tufanye mazungumzo ya haraka ili waweze kulipa dola milioni 12,830,000.
Mheshimiwa Mwenyekit, lakini baada ya kutoka hapa documents zote tulizokuwa tunafuatilia sisi kama Halmashauri mbili, ziliporwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Toka walipochukua nyaraka zile Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mpaka leo miaka mitatu hakuna kinachoendelea. Swali la kwanza, ni nini kauli yako kwa Mkuu wa Mkoa kurudisha nyaraka kwenye Halmashauri zetu kwa kuwa tuna wanasheria wazuri ili tuendelee na mchakato wa kudai fedha zetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, toka tumezaliwa tunaijua Bacliff haifanyi kazi ni utafiti usiokamilika. Miaka karibia hamsini na kitu ni utafiti usiokamilika; na kwa sasa leseni ile imeisha na kauli ya Rais ni kuzifuta leseni ambazo hazifanyi kazi ili wapewe wachimbaji wadogo na wewe mwenyewe Waziri unajisifu hapa na unaona tunavyofanya vizuri wachimbaji wadogo, tunafukuzana sasa na migodi mikubwa katika kukusanya dhahabu. Ni lini leseni hii itafutwa ili eneo lile warudishiwe wachimbaji wadogo?
Name
Doto Mashaka Biteko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Answer
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Kasheku Msukuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kulikuwa na mgogoro wa ulipaji wa service levy kwa Mgodi wa GGM pamoja na Halmashauri hizo mbili nilizozitaja za Geita Mji pamoja na Halmashauri ya Geita Vijijini. Ukweli pia ni kwamba kulikuwa na tofauti ya namna ya kukokotoa hiyo service levy, maana wao GGM mwanzo walikuwa wanalipa kwa mujibu wa MDA yao, kwa maana ya kulipa dola 200,000 kwa mwaka lakini baadaye marekebisho yalivyofanywa ya kuweka addendum kwenye MDA mwaka 2004, ikaonekana sasa malipo yaanze kulipwa kwa mujibu wa sheria yaani 0.3% ya mapato yote ya mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti hiyo imechukua muda mrefu na Serikali imekuwa ikishirikiana na Halmashauri ya Geita pamoja na Mheshimiwa Mbunge anafahamu sisi Wizara tumesukuma sana jambo hili. Hata hivyo, hapo katikati Waheshimiwa Madiwani wa Geita waliamua kupeleka jambo hili mahakamani na Mheshimiwa Mbunge anafahamu jambo hili lilishapelekwa mahakamani. Kuhusu nyaraka zile kupotezwa na nini, nadhani tuwaachie mahakama nao wao kama wanazo nadhani watazipeleka mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni lile linalohusiana na Mgodi wa Bacliff. Ni kweli kwamba Mgodi wa Bacliff umechukua muda mrefu sana na kumekuwa na matatizo mengi sana, kwanza ya kileseni lakini pili ya kiubia. Yote hayo tunayafanyia kazi na hivi navyozungumza hapa nawasiliana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuangalia namna gani ule ubia utaweza kusimamiwa, ama pengine kama kuna haja ya kuuvunja uweze kuvunjwa. Ile leseni anayoizungumzia, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini hatujatoa leseni hiyo ambayo inahitaji kuhuishwa kwa sasa, kwa sababu bado kuna mambo ambayo tunahitaji kuyakamilisha kabla ya kufanya hivyo. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved