Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rehema Juma Migilla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:- Pamoja na jitihada za vijana wengi kujiajiri wenyewe kwa kuendesha bodaboda wamekuwa wakisumbuliwa na polisi kwa pikipiki zao kukamatwa mara kwa mara:- Je, kwa nini pikipiki zao zinapokamatwa na wanapoenda kuzichukua hukuta baadhi ya vifaa kama betri hazipo?
Supplementary Question 1
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini naona majibu haya yamejibiwa kisiasa kuliko uhalisia wenyewe ulioko huko kwa waendesha bodaboda.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli ulio hai kabisa bodaboda hawa wamejiajiri wenyewe na wanafanya kazi katika mazingira magumu na wamekuwa wakisumbuliwa sana na polisi especially hawa PT. Wanawakamata na wakishawakamata hata uchunguzi wa kina haufanyiki na sometimes wanawabambikizia makosa. Wanapowabambikizia makosa wanawaaambia watoe hela, wasipotoa zile hela pikipiki zao zinapelekwa polisi. Zikifika polisi, pindi wanapotaka kuzichukua wanakuta baadhi ya vitu kama betri, mafuta na hata wakati mwingine wanakuta hadi gamba zimebadilishwa na tunaelewa kabisa polisi ni mahali ambapo pana usalama wa kutosha na hakuna mtu ambae anaweza akaenda kubadilisha kitu chochote pasipo kukamatwa.
Mheshimiwa Spika, sasa je, Mheshimiwa Waziri, unataka kutuambia wanaohusika na hili zoezi la kuchomoa vitu au vielelezo ni Polisi au akina nani na tunajua kabisa pale ni mahali salama?
Mheshimiwa Spika, swali la pili nataka kufahamu pia pamekuwa na mrundikano mkubwa sana wa pikipiki katika vituo vya polisi na ukizingatia chanzo cha kukamatwa kwa hizi pikipiki na mrundikano huo ni hawa hawa polisi wanazikamata na kuwataka hao watu walipe…
SPIKA: Sasa swali.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: … swali langu; Je, Serikali ina mpango gani kuwarudishia hawa watu pikipiki zao ambapo kwa kuendelea kukaa pale zinaidi kuharibika?
Name
Kangi Alphaxard Lugola
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwibara
Answer
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Rehema, Mheshimiwa Mbunge ambaye kwa muda mfupi tangu alipoingia Bungeni ni Mbunge machachari na nimekuwa nikimpa ushirikiano kwa masuala ya Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Spika, mwanzoni nilikuwa najiuliza kwanini watu wanaoagiza magari bandarini vitu vinachomolewa au watu kwenye viwanda vya ndege kunakuwa na pilferage lakini baadaye nikaja kushangaa hata kwenye vituo vya polisi vitu vichomolewe nikaona ni jambo ambalo linashangaza sana.
Mheshimiwa Spika, nilichofanya, kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kwenye ilani hii ya CCM Ibara ya Nne, CCM imeamua kwamba katika changamoto zile nne za Ibara ya 4 za kupunguza umaskini, za kutatua tatizo la ajira tena tukataja bayana vijana, nataka nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba bodaboda ambazo nimetoa maelekezo ili wapambane na umaskini na tatizo la ajira ni bodaboda za makundi manne tu zitakazochukuliwa kupelekwa kituo cha polisi na hata kwenye bajeti hapa nilisema.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, kundi la kwanza, ni bodaboda ambayo imehusika kwenye uhalifu, kwa sababu bodaboda zinatumika kufanyia uhalifu. Hiyo ikikamatwa itapelekwa kituoni. Kundi la pili ni bodaboda ambayo inahusika na kesi na kesi yenyewe, moja ni kama bodaboda hiyo imehusika kwenye ajali ya barabarani ama bodaboda iliyoibiwa sasa katika recovery ikawa imekamatwa, ni kielelezo. Kundi la tatu na la mwisho ni bodaboda ambayo haina mwenyewe sisi (found and unclaimed property) sasa polisi kwa sababu wanalinda mali za raia wataichukua ikae kituo cha polisi, ikipata mwenyewe ichukuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, boda boda zingine zozote ambazo hazipo kwenye kundi hilo, sijui huyu hana helmet, huyu hana side mirror, huyu amepakia mshkaki, hakuna bodaboda itakayokamatwa kupelekwa kwenye kituo cha polisi. Nimewapata utaratibu wa kuwapa siku saba kama ni faini watalipa na nimeelekeza bodaboda ambazo ziko kwenye makundi matatu ztakazopelekwa kituo cha polisi na zenyewe wataandikiwa hati inayoonesha vitu ambavyo viko kwenye bodaboda ile ili atakapokuja huyu mtu a-cross check na hati aliyopewa ili yule aliyechukua kama kuna upotevu aweze kushughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi bodaboda nchi nzima wanakula raha mstarehe, wanajinafasi. Kama Tabora suala hilo bado linaendelea, Mheshimiwa Rehema nikuhakikishie itakapofika jioni kama Tabora pale kuna pikipiki ambayo haiko kwenye makundi hayo, ama zao ama zangu. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved