Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Leah Jeremiah Komanya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Meatu
Primary Question
MHE. LEAH J. KOMANYA (k.n.y. MHE. MASHIMBA M. NDAKI) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa kila shule ya msingi au ya sekondari kunakuwa na walimu wa kike kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wa kike hasa katika masuala yanayohusiana na hedhi salama?
Supplementary Question 1
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Asilimia 10 ya EP4R inayotolewa kwa ajili ya msawazisho wa ikama, imekuwa siyo suluhu katika Mkoa wa Simiyu kwa kuwa walimu wengi sana wamekuwa wakihama. Walimu 60 wanahama kwa robo moja katika Wilaya ya Meatu na watano ndio wanahamia. Je, Serikali haioni haja ya kuwa na mkakati ili walimu wanaoajiriwa wakabaki kuitumikia Halmashauri angalau kwa miaka mitano kabla ya kuruhusiwa kuhama?
Mheshimiwa Spika, ni dhahili kwamba, siyo wasichana wote hupata hisia (pre-menstrual syndrome) kabla ya kuanza hedhi na wakati huo hakuna mwalimu yeyote wa kike ambaye anaweza kutoa msaada. Je, Serikali haioni haja ya kuwapatia Waheshimiwa Madiwani wanawake elimu ya hedhi pamoja na afya ya uzazi angalau mara moja kwa mwaka ili kwa kushirikiana na Wabunge wanawake, angalau tuwe tunatoa elimu ya uzazi kwa watoto wetu wa kike? (Makofi)
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wa Viti Maalum wote kwa kuzingatia mambo ya wanawake na hasa waschana katika shule zetu ili kuimarisha afya zao.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anapendekeza kwamba walimu ikiwezekana wakae miaka mitano ili waweze kuhudumia katika maeneo haya. Ndiyo maana Mheshimiwa Waziri Mkuu alishatoa maelekezo katika Ofisi ya Rais TAMISEMI kwamba walimu wote kwa ujumla pamoja na wahudumu wengine wa afya, tunaandaa mfumo wa kisayansi ambao utakuwa unaweza kuonyesha kama mwalimu anataka kuhama kutoka point ‘A’ kwenda point ‘B’ ikiwa tunaweza kuangalie ile ikama.
Mheshimiwa Spika, la pili, ni kwamba, tunavyozungumza hapa, mwezi huu mwanzoni, tumepeleka fedha za EP4R, motisha kila Halmashauri. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge wakafuatilie fedha zimeenda katika Halmashauri zao na kwenye majimbo yao, Halmashauri zote nchini zimepelekewa fedha hizi za ku-balance ikama, vilevile na fedha za kumalizia maboma ya shule za msingi. Naomba mkasimamie ili zifanye kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, nitasikitika sana kama kuna shule ambayo ina walimu katika Halmashauri yake, tumepeleka fedha za ku-balance ikama halafu bado iendelee kubaki shule moja ambayo haina mwalimu wa kike, itakuwa ni bahati mbaya; na kwa kweli Mkurugenzi huyo, au Afisa Elimu wa Mkoa na viongozi wa mkoa huo watakuwa hawakuitendea haki Serikali. Maelekezo ni kwamba, fedha iliyopatikana wazingatie kuhamisha walimu wa kike, wahakikishe kila Halmashauri ina mwalimu wa kike. Kwa sababu unakuta Halmashauri mbalimbali zina walimu wengi katika maeneo mbalimbali. Tulipeleka fedha ili mwalimu akihamishwa asianze kulalamika. Hili nadhani lizingatiwe na lifanyiwe kazi. Waheshimiwa Wabunge, tusaidiane kufuatilia hili ili liweze kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, hoja ya miaka mitano kuelekeza, ziko taratibu mbalimbali za Utumishi wa Umma, hizo ndizo zinazingatiwa. Hata hili la kuzuia kwa muda, kimsingi tumezuia kwa sababu baada ya malalamiko mengi, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema kwamba kuna maeneo walimu wanafika. Hata juzi tumeajiri walimu, walipaswa kuripoti tarehe 21 mwezi huu ndiyo ilikuwa waripoti kama ajira ndiyo tupange, lakini wameshaanza kuomba uhamisho. Hata kuripoti hajaripoti, hajapewa hata namna ya ajira, hajaanza kulipwa mshahara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukizuia ajira kunakuwa na malalamiko mengi sana kwamba watu wanaonewa, lakini kimsingi matatizo hayo ndiyo tunayazingatia. Kwa hiyo, tunaomba walimu waendelee kubaki maeneo yale na uhamisho umeendelea kusitishwa mpaka tutakapokamilisha mfumo ili tuweze kumhamisha mwalimu tukijua kwamba eneo analotoka au kwenda haliathiri sana utoaji wa elimu katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anashauri kwamba Waheshimiwa Madiwani wa Viti Maalum wapewe semina hii ili waweze kusaidia na Waheshimiwa Wabunge. Hili jambo tunalipokea, lakini ukweli ni kwamba elimu hii ya uzazi inatolewa; ni elimu endelevu, inatolewa kwa wazazi wenyewe, kwa wanafunzi wenyewe, kwa walimu wa kike na wa kiume. Pia Mheshimiwa Waziri wa Afya alishauri juzi hapa; na hata akina mama katika nyumba zetu, unaweza ukamlea mtoto vizuri zaidi, kwa sababu unakaa naye muda mwingi zaidi ili kusaidia kuboresha mambo haya. Tunaupokea ushauri huu, tutaona utakapofika wakati muafaka tuufanyie kazi. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved