Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Pascal Yohana Haonga
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mbozi
Primary Question
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:- Wilaya ya Mbozi ina vivutio vingi sana vya utalii, baadhi yake ni Kimondo kilichopo Kijiji cha Ndolezi Kata ya Mlangali, Majimoto na Mapango ya Popo katika Kata ya Nanyara, lakini baadhi ya vivutio hivyo hasa Majimoto na Mapango ya Popo havitambuliwi na havipo hata kwenye orodha ya kumbukumbu za Serikali:- (a) Je, ni lini Serikali itavitambua rasmi vivutio hivyo? (b) Je, kivutio cha Kimondo kimeingiza shilingi ngapi kwenye Halmashauri ya Mbozi na Serikali Kuu tangu kigunduliwe?
Supplementary Question 1
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; kwa kuwa fedha zote ambazo zinakusanywa kutokana na utalii wa Kimondo Mbozi huwa zinachukuliwa na Serikali kuu na hakuna hata shilingi moja ambayo imewahi kurejeshwa kwa wananchi wa Kijiji husika cha Ndolezi na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi: Je, Serikali haioni kwamba huu ni ubaguzi kwa wananchi wa Wilaya ya Mbozi kwa sababu maeneo mengine yenye utalii, wananchi hurejeshewa sehemu kidogo ya fedha zilizotokana na utalii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Vivutio vya Utalii vya Majimoto pamoja na Mapango ya Popo vimekuwepo kwa muda mrefu sana tangu uhuru. Je, Serikali kwa nini inaendelea kusuasua kutenga bajeti ya kuviendeleza vivutio hivi vya utalii ambavyo vipo katika Kijiji cha Nanyala, Kata ya Nanyala, Wilaya ya Mbozi?
Name
Constantine John Kanyasu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza katika swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu ni kwa nini Serikali imekuwa ikikusanya pesa hizi na kutokuzirudisha Halmashauri? Jambo hili siyo kweli.
Mheshimiwa Spika, unafahamu kwamba maduhuli yote yanayokusanywa na Taasisi mbalimbali za Setikali yanachangia katika mfuko Mkuu wa Serikali na pesa hizo ndizo zinazorudi kwa ajili ya uendeshaji wa huduma mbalimbali za jamii zikiwemo hospitali, kulipa walimu pamoja na mambo mengine na ujenzi wa miundombinu. Kwa hiyo, makusanyo haya yanayofanyika katika Serikali siyo lazima yarudi kama token kwenye Halmashauri, bali yanarudi kwa style ambayo wananchi wote katika Mkoa wa Songwe wanapata.
Mheshimiwa Spika, nimkumbushe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kimsingi jukumu la kuleta watalii na kuongeza mapato kwenye Halmashauri yake linaweza pia kufanywa na yeye. Kama mnavyofahamu, pamoja na kwamba tunapata watalii milioni 1.5 Tanzania, sehemu kubwa ya watalii hawa wanaokuja Tanzania wanatafutwa na wadau wa utalii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhamasishe Mheshimiwa Mbunge kuihamasisha Halmashauri yake na yeye mwenyewe kukitangaza kivutio hiki cha utalii, lakini pia kuweka miundombinu kwa kushirikiana na Halmashauri ili kuweza kuingiza mapato mengi zaidi kwenye Wilaya yake.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili amesema kwamba tumekuwa tukisuasua katika kutangaza Majimoto. Hatujasuasua, nimemweleza katika jibu langu la msingi Mheshimiwa Mbunge kwamba Majimoto haya na Pango la Popo tumeviingiza katika kumbukumbu za Serikali. Jukumu la kuvitangaza na kuvifanya vilete watalii linaweza kufanywa na mtu mmoja mmoja. Kama mnavyofahamu, ni kwamba sisi kama Serikali tunasimamia sera lakini jukumu la mtu mmoja mmoja linaweza kutangaza kituo kile na kuleta watalii na kuongezea Serikali mapato.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Name
Janet Zebedayo Mbene
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ileje
Primary Question
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:- Wilaya ya Mbozi ina vivutio vingi sana vya utalii, baadhi yake ni Kimondo kilichopo Kijiji cha Ndolezi Kata ya Mlangali, Majimoto na Mapango ya Popo katika Kata ya Nanyara, lakini baadhi ya vivutio hivyo hasa Majimoto na Mapango ya Popo havitambuliwi na havipo hata kwenye orodha ya kumbukumbu za Serikali:- (a) Je, ni lini Serikali itavitambua rasmi vivutio hivyo? (b) Je, kivutio cha Kimondo kimeingiza shilingi ngapi kwenye Halmashauri ya Mbozi na Serikali Kuu tangu kigunduliwe?
Supplementary Question 2
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa suala la utalii limezingatia zaidi utalii wa mbuga za wanyama na fukwe, kuna utalii ambao umesahauliwa ambao nao pia ni mzuri na unawagusa wananchi moja kwa moja; utalii wa kitamaduni.
Mheshimiwa Spika, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hususan Songwe na hata Wilaya yangu ya Ileje, tuna vivutio vingi ambavyo vingeendelezwa vingesaidia sana suala hili na wananchi wangenufaika. Tuna ngoma za jadi, tuna mila zetu na desturi, tuna aina zetu za nyumba na mavazi ambapo watalii wengi wangependa kuona, lakini tuna tatizo kubwa hatuna Maafisa Utalii katika Wilaya zetu. Tumekuwa tukiuliza mara nyingi tutafanyaje tupate Maafisa hao ili wawezeshe sasa kuboresha hii miundombinu ambayo tunaihitaji kwa ajili ya utalii wa utamaduni.
Mheshimiwa Spika, tunaomba sasa Serikali ituambie lini watatupa Maafisa Utalii ambao wamebobea katika masuala ya utalii ili watusaidie katika suala hilo?
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
Name
Constantine John Kanyasu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kama nchi, tumekuwa tukitangaza zaidi utalii wa asili kwa maana ya utalii wa safari (Mbuga za wanyama) lakini pia na utalii wa fukwe. Uko utalii wa aina nyingi sana na aina mbalimbali na labda nitumie fursa hii kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba, bado katika maeneo yote Tanzania tuna vivutio vya utalii ikiwemo ngoma za asili kama alivyosema lakini maisha yetu peke yake ni vivutio vya asili ambavyo wageni wangetamani kuona.
Mheshimiwa Spika, ushauri wa kuwa na Maafisa Utalii katika kila Halmashauri, nimekuwa nikijibu swali hili hapa mara kwa mara kwamba Wakurugenzi wetu wanapowaomba Watumishi kwenye maombi yao kila mwaka, waingize maombi ya Maafisa Wanyamapori na Maafisa Utalii kwa sababu hawa ni watu ambao watakuja ku-promote utalii katika maeneo ya Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumechukua ushauri wake, lakini niwakumbushe Wakurugenzi wote kwamba wanapoomba watumishi, waingize watumishi wenye taaluma ya utalii na wanyamapori ili kuweza kuzisaidia Halmashauri.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved