Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Devotha Methew Minja
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DEVOTHA M. MINJA (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:- Ongezeko la gharama za nishati nchini hasa umeme na gesi vimesababisha kuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya kuni na mkaa. Je, ni lini Serikali itarasimisha biashara ya mkaa ili kupunguza makali ya maisha hasa kwa Watanzania wenye kipato duni?
Supplementary Question 1
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwa na mkanganyiko wa matamko kutoka kwa Wakala wa Misitu nchini kwamba mtu akipatikana na kilo 50 za mkaa ni lazima awe na kibali maalum; ni marufuku kwa mtu kupatikana na kilo 200 za mkaa na adhabu yake ni kifungo cha miezi kumi au kulipa faini ya shilingi 50,000 na shilingi milioni 12. Hivi ni sahihi kabisa watu kama akina mama lishe, mama ntilie, akina mama wa nyumbani, adhabu hii inawahusu?
Mheshimiwa Spika, katika swali langu la pili kwa kuwa gesi siyo ajenda tena kwa Serikali hii ya wanyonge na mtungi wa gesi hivi sasa kilo 15 ni kati ya shilingi 45,000 mpaka shilingi 50,000; hivi ni kwa nini Serikali isione kuna umuhimu wa kuondoa kodi katika gesi ili kuwawezesha wananchi waweze kutumia gesi badala ya kutumia mkaa na kuni? (Makofi)
Name
Constantine John Kanyasu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Devotha Minja, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza ninakiri kwamba limekuwepo tamko kutoka ofisini kwetu linalohusiana na namna tunavyojipanga kudhibiti ukataji na uchomaji hovyo wa mkaa na tumeelekeza kwamba wahusika wa biashara ya mkaa ambao wanafanya biashara, siyo watumiaji, wahusika wa biashara ya mkaa ambao wanasafirisha mkaa kwa ajili ya kuuza wanapaswa kuwa wamepitia taratibu mbalimbali kabla ya kuchoma mkaa na taratibu hizo zinaanza katika level ya vijiji, tunaowazungumzia hapa siyo watumiaji wa mwisho kwa maana ya mama lishe na watumiaji wa ndani hawa watakwenda kununua katika maeneo maalum ambayo tumeelekeza maeneo yote yanayofanya biashara ya mkaa yatasajiliwa na wale wanaofanya biashara ya mkaa pale ndiyo watakaowauzia watumiaji wa mwisho.
Kwa hiyo, ni makosa kuwakamata watumiaji wa mkaa wa ndani ambao wamenunua kwa muuzaji ambaye ametambuliwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kweli kwamba gharama ya gesi iko juu na hii imesababisha watu wengi ku- opt kutumia mkaa na kuni hasa maeneo ya vijijini, lakini watafiti wanaonesha kwamba bado kwa gharama ya sasa matumizi ya gesi ni gharama nafuu kuliko matumizi ya mkaa. Kwa mfano sasa hivi gunia la kilo 50 la mkaa katika Jiji la Dar es Salaam linauzwa mpaka shilingi 60,000 wakati mtungi wa gesi unauzwa shilingi 50,000 na muda wa matumizi ya gesi ni muda mrefu kuliko matumizi ya mkaa.
Mheshimiwa Spika, lakini nimechukua mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge na tutajadiliana na Wizara husika kuona kama tunaweza tukaomba kuondolewa kwa baadhi ya kodi kwenye gesi ili kuhamasisha matumizi ya gesi na kupunguza matumizi kuni. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved