Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Emmanuel Adamson Mwakasaka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Primary Question
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Halmashauri nyingi zina uwezo mdogo wa kujiendesha kwa kutumia mapato yake ya ndani. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutenga fedha katika bajeti ili kuzisaidia Halmashauri kujenga hospitali na vituo vya afya badala ya kuziachia jukumu hilo Halmashauri pekee?
Supplementary Question 1
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nilikuwa naangalia kwenye haya majibu ya Serikali naona wametenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali, lakini pamoja na vituo vya afya, lakini kwenye majibu haya sijaona pesa ambayo imetengwa kwa mwaka 2019/2020 kwa ajili ya maboma ambayo yako mengi sana sehemu mbalimbali ambayo wananchi wamejitolea nguvu zao kwa ajili ya kukamilisha maboma hayo hasa ya zahanati, ujenzi wa zahanati.
Mheshimiwa Spika, sijui Serikali ina mpango gani wa kusaidia kukamilisha ujenzi wa maboma mbalimbali ambayo yamo katika sehemu mbalimbali za majimbo yetu? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Tabora Manispaa jengo la Halmashauri limechakaa sana mpaka linavuja, sehemu nyingi zinavuja, lakini Halmashauri kwa mapato yake ya ndani imejitahidi kuligharamia jengo hilo na imelipa mpaka sasa hivi zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwa mapato ya ndani na toka ujenzi umeanza mwaka 2014 Serikali imewahi kutoa shilingi milioni 450 tu katika kusaidia ujenzi wa jengo hilo. Sasa sijui Serikali ina mkakati gani wa kusaidia ujenzi wa jengo hilo ambalo ujenzi wake unafikia shilingi bilioni tano ambayo kwa mapato ya Halmashauri kama ya Tabora Mjini si rahisi kukamilisha, Serikali ina mkakati gani? (Makofi)
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, katika swali lake la mwanzo anauliza haoni fedha ambazo Serikali imetenga kwa ajili ya kumalizia maboma ambayo wananchi wametumia nguvu katika kuyajenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, msingi wa majibu katika majibu yangu ya msingi yametokana na swali alilouliza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu katika swali lake la msingi ni kama vile hakuona jitihada ambazo zinafanywa na Serikali katika kuhakikisha ujenzi wa vituo vya afya, hospitali pamoja na zahanati na ndiyo maana katika majibu ambayo nimempa nimeonesha idadi ya fedha ambazo zimetolewa na Serikali na nia njema ya Serikali ambayo inaongozwa na CCM na sisi katika Ilani yetu tumeahidi pale ambapo wananchi wanatoa nguvu yao na Serikali tunapeleka mkono kusaidiana na wananchi ili kuhakikisha nguvu ya wananchi haipotei na yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge ni shuhuda nguvu kubwa ambayo inapelekwa na Serikali kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma za afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini katika swali lake la pili kuhusiana na ujenzi pale Manispaa ya Tabora ambao unatakiwa ugharimu kama kiasi cha bilioni tano ni ukweli jengo limeanzishwa ni kubwa kweli kweli na katika hali ya kawaida kwa bajeti ya Serikali inavyotengwa si rahisi kwamba jengo hili litakamilika lote kwa mara moja na ndiyo maana tumekuwa tukiwashauri ni vizuri tukaanza upande ambao tunaweza tukaukamilisha ukaanza kutumika wakati ujenzi mwingine unaendelea kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu. (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Primary Question
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Halmashauri nyingi zina uwezo mdogo wa kujiendesha kwa kutumia mapato yake ya ndani. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutenga fedha katika bajeti ili kuzisaidia Halmashauri kujenga hospitali na vituo vya afya badala ya kuziachia jukumu hilo Halmashauri pekee?
Supplementary Question 2
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii, na mimi niulize swali dogo la nyongeza kwenye swali hili la msingi mwaka wa fedha 2017/ 2018 Serikali ilitenga shilingi bilioni 251 kwa ajili ya kumalizia majengo ya zahanati, maboma pamoja na maboma ya shule za msingi, lakini fedha hizo katika mwaka huu hawakutoa kitu na mwaka wa fedha uliofuatia 2018/2019 ambao tupo Serikali ilitoa shilingi bilioni 69 kwa ajili ya shughuli kwa maana shilingi bilioni 39 kwenye majengo ya zahanati na shilingi bilioni 28 kwenye majengo ya shule za msingi.
Sasa nataka kujua commitment ya Serikali ya shilingi bilioni 184 zilizobaki za fedha za ndani kwenda kumalizia maboma hayo ya zahanati katika nchi zetu ikiwemo Jimbo la Momba? (Makofi)
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu kwamba ukiangalia katika kipindi cha karibuni Serikali imefanya investment kubwa sana katika maeneo hayo na hasa katika upande ule wa Maboma kuna takribani shilingi bilioni 38 kwanza zilitoka kwa ajili ya sekta ya afya awamu ya kwanza, lakini juzi juzi mwezi wa tatu hapa zilitoka karibuni shilingi bilioni 29.9 kwa ajili ya sekta ya elimu.
Mheshimiwa Spika, lakini, naomba nikuhakikishie kwamba mwezi wa nne hapa katikati tumetenga tena karibuni shilingi bilioni 35.6 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba suala la sekta ya elimu kuhakikisha maboma mbalimbali yanatekelezeka.
Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo naomba nikutoe hofu Mheshimiwa Silinde kwamba Serikali ni nia yake kubwa kwamba kuhakikisha maeneo yote yenye changamoto yanaweza kufanyiwa kazi kwa lengo kubwa Watanzania wapate huduma vizuri. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved