Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. BONIFACE M. GETERE aliuliza:- Je, Serikali inachukua hatua gani endelevu za kuondoa tatizo sugu la upungufu wa madawati kwenye baadhi ya shule za msingi na sekondari nchini?
Supplementary Question 1
MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la kwanza kwenye Bunge lako hili la Kumi na Mbili.
Mheshimiwa Spika, suala la madawati limekuwa ni suala sugu sana katika nchi yetu. Swali langu la kwanza, nataka kujua Serikali ina mpango gani sasa wa kuwa na mfuko maalum au mfuko wa kudumu ambao utafanya hili tatizo la madawati liweze kupungua katika nchi yetu na hasa katika Jimbo langu la Bunda, upungufu wa madawati kwenye shule za msingi na sekondari ni mkubwa sana?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, sasa hivi nchi yetu kuna wanafunzi wanaenda shuleni hasa sekondari. Kuna mkanganyiko wa kusema twende na madawati, wengine wananunua wazazi, wengine wanasema Serikali inaleta.
Mheshimiwa Spika, nini tamko la Serikali kwenye suala hili la madawati katika shule za sekondari? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE: DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimjibu Mheshimiwa Boniface Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, maswali yake mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, ametoa kama pendekezo la Serikali kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kutatua tatizo la madawati. Jambo hili nafikiri ni jambo jema na sisi kama Serikali tunalipokea. Hata hivyo, pamoja na kupokea wazo ambalo amelileta la kuwa na mfuko maalum, lakini bado naweza kueleza kwamba hili suala la upungufu wa madawati mashuleni Serikali imeendelea kukabiliana nalo, lakini na sisi kama Wabunge tuna wajibu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, moja, kwanza sisi Wabunge ni Madiwani katika Halmashauri zetu. Pia katika halmashauri tunapswa kuwa na mipango ya kutumia fedha za ndani kuhakikisha kila mwaka tunatenga fedha kwa ajili ya kutatua tatizo la madawati.
Mheshimiwa Spika, vilevile sisi ni Wenyeviti wa Mifuko ya Jimbo. Kwa hiyo, kama kuna changamoto katika halmashuri yako sehemu ya fedha za Mfuko wa Jimbio unaweza kuzitumia katika kutatua tatizo la madawati. Aidha, unaweza kutafuta wadau mbalimbali ambao wanaweza kusaidia kuhakikisha kwamba tunaondoa changamoto hiyo.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusiana hoja kwamba watu wengi wamekuwa wakilazimishwa ili mwanafunzi aingie darasani lazima mpaka ulipe mchango wa dawati ama utoe dawati. Msimamo wa Serikali ambao aliutoa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni kwamba wanafunzi wote wanapaswa kujiunga bila kuwa na masharti, kama hilo linaloletwa la kusema kwamba lazima mtu atoe dawati ndiyo asajiliwe shuleni.
Kwa hiyo, msimamo wa Serikali bado uko palepale na tutaendelea kusimamia huo msimamo wa Serikali kama ambavyo Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameagiza. Ahsante sana.
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Primary Question
MHE. BONIFACE M. GETERE aliuliza:- Je, Serikali inachukua hatua gani endelevu za kuondoa tatizo sugu la upungufu wa madawati kwenye baadhi ya shule za msingi na sekondari nchini?
Supplementary Question 2
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kila baada ya miaka 10 tumekuwa tukifanya sensa ambapo sensa hii pamoja na mambo mengine inaonesha mtawanyo wa umri na kwa hiyo, ni rahisi kufanya maoteo ya watoto wanaoingia shuleni. Kwa kuwa, tatizo hili la mawati limekuwa likitokea kila mwaka inapotokea tunaanza msimu mpya wa masomo, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kutumia takwimu zinazotokana na sensa kujiandaa vizuri kulimaliza tatizo hili badala ya kutokea mwaka hadi mwaka? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Nnauye, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimuondoe hofu, Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inatumia takwimu sahihi kuhakikisha kwamba tunakabiliana na changamoto za madawati na wanafunzi mashuleni. Ndiyo maana nimeeleza katika moja ya mpango wa Serikali ambao sasa hivi upo ni kwamba kila darasa linavyokuwa linajengwa ni lazima liwe na madawati ama kama ni shule lazima iwe na miundombinu yote. Kwa hiyo, hiyo ni sehemu tu ya kuhakikisha kwamba tunakabiliana na changamoto ya madawati mashuleni.
Mheshimiwa Spika, lakini pili na kwa kifupi ni kwamba sisi tuna huo mpango na nimhakikishie kabisa kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano, hiyo kero ya madawati mashuleni tunayo na tutaieleza katika mpango wetu wa bajeti wakati utakapofika.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved