Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maimuna Salum Mtanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Primary Question

MHE. MAIMUNA S. MTANDA Aliuliza:- Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina Kata 22 na Vijiji 107, lakini ina Vituo vya Afya vitatu tu, kati ya 22 vinavyohitajika. Je, Serikali haioni haja ya kujenga Vituo vipya vya Afya katika Halmashauri ya Newala ili kuboresha huduma za Afya kwa wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Jimbo la Newala Vijijini linakabiliwa na uhaba mkubwa wa upatikanaji wa dawa kwa wananchi wake. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na suala hili? Uhaba ule unachangia kwa kiasi kikubwa sana wananchi kushindwa kujiunga na mpango wa CHF iliyoboreshwa kwa sababu wamekatishwa tamaa na mpango wa awali, wakienda vituoni hawapati dawa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Jimbo la Newala Vijijini linakabilishwa na uhaba mkubwa pia wa watumishi, hali ambayo inazorotesha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi. Ni lini Serikali itapeleka watumishi wa afya katika Jimbo la Newala Vijijini ili wananchi wale wapate huduma inayostahili kama wananchi wengine? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeweka kipaumbele kuhakikisha vituo vyetu vya huduma kote nchini vinakuwa na dawa za kutosha. Ndiyo maana katika kipindi cha miaka mitano, bajeti ya dawa ya Serikali imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 271 mwaka 2020. Hii ni jitihada kubwa sana ya Serikali kuhakikisha wananchi wanapata dawa za kutosha vituoni.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusisitiza, kwanza kuhakikisha Halmashauri zinasimamia ipasavyo mapato ya uchangiaji wa huduma za afya katika vituo vyetu. Nasi Waheshimiwa Wabunge ni sehemu ya Madiwani katika Halmashauri zetu, kumekuwa na changamoto ya usimamizi wa makusanyo ya fedha za uchangiaji ili ziweze kuongeza mapato ya vituo na kuboresha dawa katika vituo vyetu. Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu na kuboresha upatikanaji wa dawa nchini kote lakini katika Halmashauri ya Newala Vijijini.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na uhaba wa watumishi, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele cha hali ya juu sana katika kuboresha upatikanaji wa watumishi katika vituo vyetu. Mipango iliyopo ni pamoja na kuendelea kuajiri na ushahidi unaonekana. Katika kipindi cha miaka mitano, zaidi ya watumishi 14,000 na mwaka jana madaktari 1,000 wameajiriwa katika vituo vyetu mbalimbali. Zoezi hili la kuajiri watumishi wa afya ni endelevu na Serikali itaendelea kuajiri ili kuboresha huduma za afya katika nchi yetu.