Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Pius Stephen Chaya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Mashariki
Primary Question
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti ili kubaini uwepo wa aina mbalimbali za madini katika Jimbo la Manyoni Mashariki hususan Kata za Sasilo, Makuru, Kintinku na Solya?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Madini. Nina maswali mawili ya nyongeza. Wewe mwenyewe unatambua kwamba Sekta ya Madini ina mchango mkubwa sana kwenye kukuza ajira kipato na Pato la Taifa. Swali la kwanza, je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuja na utafiti wa kina ili tuweze kuibua taarifa za kijiolojia zitakayoisaidia Serikali kuwekeza kwenye mambo ya madini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tayari Naibu Waziri amesema kuna Taarifa za awali kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo Kata ya Makuru, katika Kijiji cha Londoni ambako tayari wachimbaji wa madini wadogo wadogo wanachimba. Sasa, je Serikali imejipanga vipi kuwawezesha wananchi katika maeneo ambayo kuna taarifa za awali ili waweze kujikita kwenye uchimbaji wa madini, tukuze ajira na kipato cha nchi? Ahsante.
Name
Prof. Shukrani Elisha Manya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba utafiti wa kina ndilo jawabu la hatimate kuwezesha uchimbaji kufanyika. Sasa mojawapo ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ambayo yanaonesha tumaini na huko mbele ni pamoja na kuziwezesha Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Madini kwa rasilimali ili ziweze kufanya majukumu yake ipasavyo. Ni katika mtindo huo huo kwamba Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia ya Madini - GST imepokea vifaa rasilimali kama wiki mbili zilizopita tulipata magari sita kwa ajili ya kuwawezesha kufanya ugani.
Mheshimiwa Spika, pia STAMICO wamewezeshwa na wao wenyewe kwa pato lao la ndani wamepata mitambo mitatu ya drilling. Sasa hizo ni hatua za kuimarisha Taasisi ili hatimaye ziweze kufanya kazi ya utafiti wa kina na hatimaye kuwasaidia wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu swali lake la pili linauliza ni lini watawezeshwa; ni katika mtindo huo wa kwamba tutakapokuwa tumeendelea zaidi kuimarisha taasisi zetu kwa uwezo wa kifedha kama ambavyo Serikali imeanza kufanya tunapenda kuamini kwamba tunaelekea mahali ambapo Taasisi ya Jiolojia inaweza ikashirikiana na STAMICO na hatimaye wakawa wanafanya utafiti wa kina mahali fulani na kwa utafiti huo sasa wakapewa wachimbaji wadogo ili waweze kufanya kazi zao kwa tija. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved