Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Deus Clement Sangu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Primary Question
MHE. DEUS C. SANGU Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi uliopo katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Pori la Akiba la Uwanda?
Supplementary Question 1
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; katika operesheni za askari wa Wanyamapori kumekuwa na tabia ya askari kunyang’anya wananchi mali ikiwemo mashine za boti, mikokoteni na mali nyingine za wananchi. Nataka kujua kauli ya Serikali ni nini kwa sababu askari hawa wamekuwa wakizikamata hizo mali, wanakuwa nazo zaidi ya miaka miwili mpaka mitatu, ambayo hiyo ni hasara kwa Serikali na kwa wananchi kuwasababishia umaskini?
Swali la pili; naomba kutokana na unyeti wa tatizo hili na hali kuwa tete katika maeneo haya; je, Naibu Waziri yuko tayari kama Wizara kuja baada ya Bunge hili ili wajionee uhalisia wa jambo hili?
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya kisheria yanapokuwa yako chini ya kimahakama, sisi kama wahifadhi tunategemea zaidi Mahakama jinsi itakavyoamua. Kwa hiyo, ushahidi mara nyingi lazima ubaki kama kielelezo tosha pale ambapo kesi inapopelekwa Mahakamani, basi ushahidi utolewe ukionyesha na vitu ambavyo amekamatwa navyo mtuhumiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala hili, kwa kuwa mhimili wa Mahakama ni sehemu nyingine tofauti na mhimili wa Wizara ya Maliasili na Utalii, hivyo kwenye masuala ya kisheria tunayaacha yanaendeshwa kisheria na vifaa vyote ambavyo amekamatwa navyo mtuhumiwa inakuwa kama ushahidi, hivyo vinaendelea kutumika mpaka pale ambapo Mahakama inakuwa imeshatoa maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine la kuamba na Mbunge, Wizara iko tayari na tutaenda kuangalia hiyo migogoro iliyoko katika eneo hilo na tutalisuluhisha kadri itakavyowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Name
Dr. John Danielson Pallangyo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Mashariki
Primary Question
MHE. DEUS C. SANGU Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi uliopo katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Pori la Akiba la Uwanda?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona na mimi.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zilizoko kule Kwela, zinafanana sana na kule Arumeru Mashariki hususan Kitongoji cha Momela ambacho kimepakana na Hifadhi ya Arusha National Park.
Je, Serikali inasemaje kuhusu ule mgogoro ambao umedumu kwa miaka kama mitano sasa hivi, wananchi walikuwa wanaishi kwenye yale mashamba, baada ya ukomo wa umiliki kumalizika, baadae wakaja kuondolewa kwa nguvu?
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema awali kwamba Serikali kwa kutambua umuhimu wa wananchi wake na jinsi ambavyo kumekuwa na migogoro ya ardhi hasa upande wa mipaka ya hifadhi, iliteua Kamati ya Mawaziri nane ambao walitembelea maeneo yote ya hifadhi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hii tayari imeshamaliza mchakato wake na tumeshaanza kukaa kwa ajili ya kuangalia namna ya kutatua migogoro hii. Namwomba Mheshimiwa Dkt. Pallangyo awe na subira maana Kamati hii tayari imeshaanza kazi na baada ya Bunge lako tukufu hili utekelezaji wake sasa utaanza. Kwa hiyo, sehemu zote ambazo zina migogoro ya mipaka inaenda kutatuliwa na pale ambapo kuna migogoro mipya itakayoibuka, basi Serikali itaona ni utaratibu gani mwingine ambao itafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu rai kwa maeneo mengi nchini ambayo yanakutana na hii changamoto ya mipaka na migogoro ya hifadhi, mara nyingi kumekuwa na tatizo kubwa sana la wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi. Maeneo haya kwa asilimia kubwa ni njia za wanyama (shoroba). Kwa hiyo, migogoro mingi tunaianzisha kwa maana ya wananchi kupewa maeneo, lakini kwa upande wa pili tena tunaanzisha mgogoro mwingine wa wanyama wakali kupambana na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, tuwe na hiyo tahadhari pia kwamba tunapokuwa tunayaachia maeneo, lakini tunakuwa tumeanzisha mgogoro mwingine tena kati ya wanyama na binadamu. Maana wanyama siku zote wanapita maeneo yale yale ambayo walizaliwa nayo mwanzo na waliwaacha mabibi na mababu zao pale. Kwa hiyo, hili tatizo litaendelea kuwepo tu kama wananchi wenyewe hawatakubali uhifadhi ubaki kuwa hifadhi na maeneo mengine ya wananchi yaendelee kutumika kwa wananchi wa kawaida. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved