Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI Aliuliza:- Je, ni lini Daraja la Kisorya – Lugezi litakalounganisha Wilaya za Bunda na Ukerewe litajengwa ili kurahisisha ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Wilaya hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa jibu la Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua jitihada za Serikali kuboresha usafiri kati ya Rugezi kwenda Kisorya. Hata hivyo, kutokamilika kwa hili eneo la Lot III na hasa barabara ile ya kilometa 14 kutoka Rugezi – Nansio inaathiri sana uchumi wa wananchi wa Ukerewe, na ndiyo maana tarehe 04 Septemba, 2021 Hayati Dkt. John Magufuli akiwa Ukerewe, kwa kutambua changamoto hizi alitoa maelekezo eneo hili lifanyiwe kazi mara moja. Mwaka jana Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa Ukerewe alisisitiza jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwanini sasa Wizara isione umuhimu wa jambo hili ikatenga pesa kwa haraka ikaufanya kama mradi wa haraka ili Lot III, hasa wakati wanasubiri pesa za kujenga daraja basi barabara km. 14 kati ya Rugezi kwenda Nansio iweze kukamilika kwa haraka?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi Mbunge wa ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Ukerewe. Lakini Mheshimiwa Mbunge yeye pia atatambua kwamba Serikali inafanya jitihda kubwa sana kuhakikisha kwamba inatengeneza barabara na ndiyo maana imegawanywa kwenye Lot III. Lot ya pili imeshakamilika, lot ya kwanza mkandarasi yuko site na Serikali imeahidi kwamba inatafuta fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, daraja tunaloliongelea urefu wake unafanana na daraja karibu lile linalojengwa la pale Surrender Bridge, ni takriban kilometa moja. Kwa hiyo Serikali lazima ihakikishe kwamba inajitahidi kupata fedha ya kutosha ili kuweza kujenga daraja hilo; na ndiyo maana tayari usanifu wa kina umeshafanyika. Tayari Serikali imeonesha jitihada za makusudi, kwamba kwanza ni ahadi ya Hayati Rais, lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa hiyo Serikali kama nilivyosema kwenye jibu la msingi inaendelea kutafuta fedha na fedha ikipatikana nina uhakika kipande hiki cha Lot ya tatu kitajengwa. Ahsante.

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI Aliuliza:- Je, ni lini Daraja la Kisorya – Lugezi litakalounganisha Wilaya za Bunda na Ukerewe litajengwa ili kurahisisha ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Wilaya hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tuko katika Wizara ya Ujenzi, na Wizara hii ndiyo inayoshughulikia barabara pamoja na madaraja, sasa nilitaka kuuliza swali linalohusu barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitutembelea kule Milola na tukampa kero yetu ya barabara ambayo inatoka Ngongo inapitia Rutamba, Milola hatimaye inamalizikia Ruangwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu alituahidi kwamba barabara ile itajengwa kwa kiwango cha lami.

Sasa, je, ni lini barabara ile itajengwa kwa kiwango cha lami?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongezala Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu ipo kwenye mipango, na ninaamini usanifu wa awali unaweza ukaanza kwa sababu hatujapita bado kwenye bajeti. Niombe kujiridhisha, Mheshimiwa Salma nimuombe baada ya kikao hiki pengine tuweze kukutana naye ili tuweze kuona barabara hii iko kwenye mpango kwasababu sasa hivi tuko bajeti kwa hiyo ni ngumu kusema barabara hii iko kwenye hatua gani. Kama ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kama iko kwenye ilani naamini itakuwa ni barabara ambazo ziko kwenye matazimio ya kufanyiwa kazi na hasa upembuzi yakinifu. Ahsante.

Name

Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI Aliuliza:- Je, ni lini Daraja la Kisorya – Lugezi litakalounganisha Wilaya za Bunda na Ukerewe litajengwa ili kurahisisha ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Wilaya hiyo?

Supplementary Question 3

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuwa barabara inayoanzia King’ori, hadi Ngarenanyuki imekuwa kero kubwa sana kwa wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, na Serikali imekuwa ikiahidi mara nyingi kujenga barabara ii katika kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka kufahamu ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi yake kwa wananchi wa Arumeru Mashariki?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Magige kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba ni lini barabara ya Kilole kwenda Ngarenanyuki itajengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hizi zote ambazo zimeainishwa tuna uhakika tutazikamilisha katika kipindi hiki cha miaka mitano. Lazima kutakuwa na mahali tutaanza na barabara chache lakini tutamaliza zote. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara zote ambazo zimeainishwa na ambazo zimeahidiwa zipo kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Kipaumbele ni zile barabara ambazo zinaunganisha mikoa na mikoa, wilaya na wilaya. Ahsante.

Name

Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI Aliuliza:- Je, ni lini Daraja la Kisorya – Lugezi litakalounganisha Wilaya za Bunda na Ukerewe litajengwa ili kurahisisha ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Wilaya hiyo?

Supplementary Question 4

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Iringa Mjini kupitia Jimbo la Kalenga kwenda Kilolo kilometa 133 ambayo ina madaraja ni barabara ambayo ilikuwa ni ahadi ya hayati Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, alipofika pale akatoa ahadi hiyo, ni miaka mitano sasa imepita haijafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni lini Serikali itaijenga barabara hii ili angalau kumuenzi hayati kwasababu alienda akaona wananchi wa kule wanavyohangaika katika kuuza mazao yao kwenda katika sehemu mbalimbali?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Grace kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii yenye urefu wa km. 133 iliyoko Mkoani Iringa na ambayo ni ahadi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Hayati, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli naomba nimhakikishie kwamba Serikali haitaacha ahadi zote ambazo zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais. Nataka nimhakikishie kwamba barabara zote ambazo zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais ikiwa ni pamoja na hiyo zitajengwa kwa kiwango cha lami awamu kwa awamu. Ahsante.