Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Husna Juma Sekiboko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO K.n.y. MHE. RASHID A. SHANGAZI Aliuliza:- Je, ni vigezo gani hutumika kushindanisha ufaulu kwa shule za msingi na sekondari kwa Halmashauri na Mikoa hapa nchini?
Supplementary Question 1
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili ufaulu mzuri uweze kupatikana inategemea sana mazingira ya kujifunzia na kufundishia hasa ikama nzuri ya walimu.
Je, Serikali haioni kwamba sio haki kuwashindanisha au kushindanisha Halmashauri za Mjini na Vijijini ambako kuna mazingira magumu ya kujifunzia na kufundishia na kuna uhaba mkubwa wa walimu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali haioni ni wakati sahihi sasa kutazama upya vigezo hivi vya kuzingatia katika kupanga madaraja haya ya ufaulu kwa kuwa kwa kuzingatia maeneo hayo ya mjini na vijijini ambako shule za vijijini zina mazingira magumu sana ya kujifunza na kufundishia ukilinganisha na shule za mjini?
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sekiboko kwa niaba ya Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba tuna changamoto kubwa ya walimu kwenye shule zetu na mwaka jana mwezi Novemba, Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI ilifanya uajiri wa walimu zaidi ya 8,000 na maeneo makubwa ambayo yali-focus au walipelekwa walimu wale ni maeneo ambayo yenye changamoto kubwa sana ya walimu hasa hasa kule vijijini na maeneo ya pembezoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa suala la ikama ya walimu nipende tu kusema kwamba Serikali bado tunafanyia kazi, kuna walimu wengine zaidi ya 5,000 ambapo kupitia Wizara ya TAMISEMI tunaratajia hivi punde walimu hao watasambazwa kwenye maeneo hayo ili kuweza kusawazisha ile ikama na kuondoa changamoto hii ya upungufu wa walimu kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la utaratibu wa madaraja, utaratibu huu wakupanga madaraja katika ngazi ya shule na kwa wanafunzi wetu imezingatia vigezo vya kitaifa, kikanda na kimataifa. Kwa hiyo tukisema kwamba leo hii tuweze kubadilisha vigezo hivi kwa sababu tu kuna shule ambazo hazina ikama ya walimu itakuwa hatutendei haki kwenye eneo letu hili la kutoa elimu kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nadhani eneo kubwa la kujikita ni pale kwenda kuhakikisha kwamba ikama ya walimu inapatikana, lakini kwa upande wa vigezo hivi vilivyowekwa imezingatia sana ubora wa elimu yetu na katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Naomba kuwasilisha.
Name
Furaha Ntengo Matondo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO K.n.y. MHE. RASHID A. SHANGAZI Aliuliza:- Je, ni vigezo gani hutumika kushindanisha ufaulu kwa shule za msingi na sekondari kwa Halmashauri na Mikoa hapa nchini?
Supplementary Question 2
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali.
Kwa kuwa mazingira ya jiografia ya Wilaya ya Ukerewe yanaathiri sana ufaulu wa Watoto wa kike, kwa nini sasa Serikali isione umuhimu wa kujenga shule maalum ya bweni katika Wilaya ya Ukerewe?
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nipende kujibu swali la Mheshimiwa Furaha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna changamoto za watoto wa kike sio tu kwa upande wa Ukerewe bali kwa maeneo mengi ya nchi yetu. Nipende kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna programu mbalimbali ambazo zitawezesha sasa kwenye maeneo mengi ambapo tuna changamoto ya vijana wetu kutembea umbali mrefu kuweza kupata shule za bweni katika maeneo hayo.
Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge Serikali iko mbioni sasa katika mpango wake wa P4R kuhakikisha tunaweza kwenda kujenga shule kwenye maeneo ambayo yana changamoto kama hizi ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu, ahsante.
Name
Kenneth Ernest Nollo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bahi
Primary Question
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO K.n.y. MHE. RASHID A. SHANGAZI Aliuliza:- Je, ni vigezo gani hutumika kushindanisha ufaulu kwa shule za msingi na sekondari kwa Halmashauri na Mikoa hapa nchini?
Supplementary Question 3
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika,naomba kuuliza swali la nyongeza, kigezo kikubwa cha ufaulu cha wanafunzi kwenda kidato cha kwanza au kwenda kidato cha tano imekuwa ni zile grade aidha A,B,C ambazo zinatumika sasa katika ufaulu, lakini kwenye midterm reviews za wanafunzi hasa mitihani Serikali imekuwa na utaratibu ambao tumeendelea nao nadhani tulirithi kwenye ukoloni kwa kutoa wa kwanza mpaka wa mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili limekuwa lina- affect watoto kisaikolojia na mtoto anakuwa na alama A, lakini ni wa kumi na ukimuuliza ulikuwa wangapi darasani anakwambia nilikuwa wa kumi lakini ana A; je, Serikali haioni jambo hili linaathiri watoto kisaikolojia na katika maisha mtu kujiona kwamba yuko grade ya mwisho? (Makofi)
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nollo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna uhakika sana kama kuwapanga watoto wa kwanza mpaka wa mwisho kuna haribu saikolojia ya watoto bali inaonesha ushindani na namna gani watoto wanaweza wakashindana ili kuweza na yeye kujisukuma kuweza kufika hapo juu, lakini nadhani ni suala ambalo linahitaji kufanyiwa utafiti kwamba je, kupangwa watoto katika utaratibu huo kuna athiri kisaikolojia. Hili naomba tulibebe tukalifanyie utafiti na kama tukiona kama kweli lina tija tunaweza tukaja kutoa majibu mbele ya Bunge lako tukufu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved