Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO K.n.y. MHE. ALLY J. MAKOA Aliuliza: - Je, ni lini Serikali itakarabati au kujenga Hospitali mpya ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa kwa kuwa Hospitali iliyopo ni ya muda mrefu na miundombinu yake ni chakavu?
Supplementary Question 1
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi ya ukarabati katika hospitali mbalimbali kongwe hapa nchini lakini bado kumekuwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa afya.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba mapungufu hayo yanakidhi haja iliyopo kwa maana ya idadi ya watumishi wanaotakiwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ujenzi wa hospitali au ukarabati wa zahanati, vituo vya afya na hizo hospitali ni pamoja na kuhakikisha mambo muhimu ya madawa, vitendanishi vinapatikana katika hospitali zetu. Je, Serikali inahakikisha vipi kwamba upatikanaji wa madawa yote muhimu yanapatikana katika hospitali zetu na katika vituo vya afya na zahanati zetu. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali kwa kuwajali na kuthamini sana afya za wananchi imeendelea kujenga vituo vya afya kote nchini na kwa kweli kuna upungufu wa watumishi kwa takribani asilimia 45. Serikali imeweka mipango thabiti ya kuhakikisha tunaendelea kuajiri watumishi katika vituo vya afya, zahanati na hospitali za Halmashauri na ndiyo maana mwezi wa Tano hadi wa Sita tulikuwa na ajira za watumishi wa afya 6,324 na watumishi hao wamekwisha ajiriwa tayari wamepelekwa kwenye vituo vya huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, zoezi hili la kuendelea kuajiri watumishi ni endelevu, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua na itaendelea kuhakikisha kwamba inaajiri watumishi kwa awamu ili kupunguza uhaba wa watumishi katika vituo hivyo.
Mheshimiwa Spika, pili; ni kweli kwa sababu ya ongezeko la vituo vya huduma za afya kumekuwa na upungufu wa baadhi ya dawa muhimu katika vituo vyetu na Serikali imeendelea kupeleka fedha Bohari Kuu ya Dawa mpaka Juni tarehe 30 mwaka huu, jumla ya bilioni 120 zilikuwa zimepelekwa Bohari Kuu ya Dawa kwa ajili ya kununua dawa kupeleka katika vituo vyetu.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha 2021/ 2022 fedha zimetengwa zaidi ya bilioni 280 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba dawa zinapelekwa katika vituo vyetu. Kwa hivyo, nimhakikishie kwamba suala hilo litaendelea kutekelezwa kwa ufanisi unaotakiwa ili dawa zipatikane katika vituo vyetu. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved