Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwantatu Mbarak Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Primary Question

MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS Aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuwainua Watu Wenye Ulemavu kwa kuwapatia vifaa vya michezo na walimu ili waweze kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa?

Supplementary Question 1

MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kabla ya kuuliza swali la nyongeza kwanza nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali kwa jitihada za kuona umuhimu wa kusaidia kuimarisha shughuli za michezo kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2021/2022, Bunge liliidhinisha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya shughuli za michezo. Je, kwa bajeti hii, kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya kuendeleza shughuli za michezo kwa watu wenye ulemavu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliiagiza Wizara kuimarisha michezo kwa wanawake na nimeona katika vyombo vya habari kwamba Wizara inajiandaa kutayarisha tamasha ambalo litajumuisha wanamichezo wanawake wa Tanzania nzima. Niipongeze sana Wizara kwa kufanikisha hilo. Swali langu, kwa vile michezo hii inajumusiha wanawake wa Tanzania nzima, je, maandalizi yamezingatia vipi ushiriki wa wanawake wakiwemo wanawake wenye ulemavu kutoka Zanzibar? Ahsante. (Makofi)

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza amehitaji kufahamu katika Mfuko wetu wa Maendeleo ya Michezo ambao Bunge hili Tukufu mmetupitishia zaidi ya 1.5 billion, je, fedha hizi zitakwenda kuwa-support watu wenye ulemavu? Naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba watu wenye ulemavu katika Wizara yetu ni watu wa kipaumbele. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi kabisa kwamba pale ambapo watakuwa wanahitaji support ya Wizara, hasa kwa michezo ya Kimataifa ndiyo sababu ya fedha hizi kupitishwa na sisi tutaendelea kuwapa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, pia siyo fedha hizi tu tuna fedha kwa ajili ya Mfuko huu kupitia michezo ya bahati nasibu, maana yake mfuko huu utaendelea kutunishwa. Kabla ya hapo fedha zilikuwa chache, tulikuwa na takribani zaidi ya milioni 200 kwenye Mfuko kwa ajili ya kuwa-support, lakini kwa sasa kwa fedha hizi maana yake wao watakapofuzu kupitia kwenye vyama vyao sisi tutaendelea kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, alihitaji kufahamu kwenye tamasha hili la michezo kwa wanawake ambayo Wizara yetu jana pia tumezindua Kamati ya kusimamia tamasha hili ambalo litasimamia michezo kwa wanawake, je, watu wenye ulemavu wamepewa nafasi kiasi gani.

Naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba watu wenye ulemavu katika tamasha hili watashiriki kupitia michezo yao ambayo wanacheza. Kwa sasa kuna timu ya mpira wa kikapu na wanariadha watashiriki katika tamasha hili na pia tumeshirikisha wote.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe rai kwa Watanzania wote hili tamasha litakapoanza mwezi huu wa Septemba kuanzia tarehe 16 na kuendelea, tushiriki kwa pamoja ili tuweze kumuenzi Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwenye suala zima la kunyanyua wanawake katika michezo. Nitoe rai kwa Wabunge wenzangu, tutaleta mwaliko kwako Spika, naomba tushiriki. Najua tunacheza netball, lakini kamba na michezo mingine wanawake tujitokeze na tamasha hili litakuwa endelevu.