Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Daniel Awack Tlemai
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karatu
Primary Question
MHE. DANIEL A. TLEMAI Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro wa mpaka kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Kata ya Mbulumbulu katika Kijiji cha Lositete?
Supplementary Question 1
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilianzishwa mwaka 1959 na mgogoro uliopo umekuja mwaka 2003 ambao umeweza kuchukua maeneo ya wananchi wa eneo hili la Kata ya Mbulumbulu, Kijiji cha Lositete. Sasa ni nini majibu ya Serikali kwa sababu mwaka 1959 kuanzishwa kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, hakukuwa na mgogoro, lakini mgogoro umekuja baada ya marekebisho ya mwaka 2003.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, ni lini Waziri yuko tayari kuongozana nami ili ajionee katika maeneo ya Kata ya Mbulumbulu, eneo la Lositete ili kuona kwamba wananchi jinsi wanavyopata shida katika eneo hili la Lositete? (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daniel Awack, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati hifadhi hizi zinaanzishwa mwaka 1959, wilaya zilikuwa ziko ndani ya wilaya za zamani. Kwa mfano; Karatu ilikua ndani ya Mbulu na sasa hivi Karatu iligawanywa, lakini pia na Ngorongoro ni Wilaya, kuna Monduli na kadhalika. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba haya maeneo yalienda kutafsiriwa na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa pamoja na Wilaya na walishirikishwa wananchi kutambua ile mipaka.
Mheshimiwa Spika, huu mpaka ambao unagombaniwa ni mpaka ambao ni wa muhimu sana kiuhifadhi; kwanza unatunza maji, unatunza mazingira, lakini pia, hawa wananchi walioko kwenye maeneo yale wanang’ang’ania kuingia mle kuchunga mifugo yao. Hatari itakayojitokeza ni kwamba maeneo mengi tunaenda kuyamaliza na tutasababisha kuwepo na tatizo la kukosa maji na wananchi katika maeneo yale wataweza kuathirika.
Mheshimiwa Spika, niwaombe wananchi watambue kwamba Serikali ina nia njema ya kutunza vyanzo vya maji kwa ajili ya jamii zinazozunguka maeneo hayo. Pia eneo lile tumelihifadhi kwa ajili ya Hifadhi ya Ngorongoro ambapo kuna eneo ambalo ni msitu ambao unahifadhiwa kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji kwa ajili ya wenyeji waliomo ndani yake. Niwaombe sana wananchi watambue kwamba Serikali ina nia njema na inawapenda ndiyo maana inahifadhi maeneo haya kwa ajili ya maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Spika, ombi lake la pili la kuongozana na mimi, nimtoe wasiwasi tutaongozana wote kama ambavyo nimefanya kwenye ziara zangu nyingi baada ya Bunge la mwezi wa Sita kuisha, kwa hiyo tutakwenda pamoja. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved