Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Primary Question

MHE. TUMAINI B. MAGESSA Aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje katika kupanga matumizi bora ya ardhi kwa Vijiji vyote nchi nzima ili kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi?

Supplementary Question 1

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ardhi, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa vile Wizara ya Ardhi kupitia Tume ya Mipango ya Ardhi inasimamia na kuratibu shughuli za matumizi bora ya ardhi; na kutokana na kwamba Tume hii imeshafanya matumizi bora ya ardhi kwenye hatua tofauti tofauti, lakini maeneo mengi nchini hayajafikishwa kwenye hatua ya mwisho na hivyo kuwachanganya wananchi kwamba, matumizi bora ya ardhi yaanze kutumika au yasitumike: Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya kukamilisha matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo ambayo wamekwishaanza kuyapanga sasa?

Swali la pili; inaonekana wazi kwamba Wizara inahamasisha Halmashauri zitenge fedha: kwa kuwa Tume hii ambayo sasa inaonekana wanaendelea na huku Wizara inahamasisha tu; na kuhamasisha siyo kumlazimisha mtu, inakuwa siyo wajibu, yaani Halmashauri haiwajibiki moja kwa moja: Je, Serikali haioni kwamba sasa itoe nyaraka ambayo inaweza kuifanya kila Halmashauri itenge fedha hizi kila mwaka kwa ajili ya kutenga matumizi bora ya ardhi katika maeneo waliyonayo?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza Mheshimiwa Tumaini anasema: Je, Wizara haioni umuhimu wa kukamilisha mpango wa matumizi katika yale maeneo ambayo yamekwishaanza?

Mheshimiwa Spika, ni kweli swali lake ni la msingi. Changamoto tunayoipata ni kwamba katika suala zima la uanzishwaji maeneo mapya, unaweza ukawa na kijiji ambacho tayari kilishafanyiwa mpango wa matumizi na wakaanza kuutumia, lakini baadaye tunapogawa maeneo unakuta tena kile kijiji kinakatwa. Kwa hiyo, ule utekelezaji wa ile mipango ya awali inashindikana kufanyika, inabidi kuanza upya.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai tu kwa Halmashauri zote nchini ambazo ndiyo mamlaka za upangaji, pale ambapo vijiji tayari vinakuwa vimeshawekewa mpango wa matumizi, tunaomba sana sana sana visifanyiwe mgawanyiko wowote. Kwa sababu, kitendo cha kugawanya kijiji kile kinaharibu mpango mzima, inabidi kuanza upya. Kwa hiyo, tumejikuta kuna vijiji tayari vilishafanyiwa mpango, lakini matumizi yake sasa yanashindikana kwa sababu kumezaliwa kijiji kingine ndani ya kijiji kingine. Kwa hiyo, naomba hilo liangaliwe katika Mamlaka zetu za Upangaji, nasi Wizara tutakuwa makini katika kufanya ufuatiliaji wa karibu.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anauliza kuhusu kuzitaka Halmashauri zitenge bajeti; pengine wanajivutavuta katika suala hilo, lakini nataka nimtie tu shime kwamba Wizara haijanyamaza katika hilo. Katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi 1,500,000,000/=, kwa ajili ya kusaidia katika shughuli hiyo ya upangaji wa matumizi, lakini hii haiondolei Mamlaka husika za Upangaji kutotimiza wajibu wake. Kwa hiyo, bado tunasisitiza kila Halmashauri ya Wilaya ihakikishe katika vitengo vyake, inapopanga bajeti za maendeleo, waikumbuke sekta ya ardhi kuitengea bajeti ya kutosha. Kwa sababu ardhi usipoipangia matumizi ndiko huko ambako migogoro inaanzia.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara tunaingia katikati kuweza kusukuma hili jukumu liende, kwa sababu tunasimamia miongozo na nyaraka mbalimbali ambazo zinasukuma uendelezaji wa sekta ya ardhi. Kwa hiyo, ninachotaka au tunachoelekeza, Halmashauri zenye mamlaka, hili ni jukumu lao la msingi kuhakikisha upangaji, upimaji na umilikishaji unafanyika, kuhakikisha vijiji vyote vinakuwa na mpango wa matumizi ya ardhi, kwa kutenga bajeti stahiki na Wizara tutakuwa tayari kuendelea kuwasaidia. Kama ambavyo sasa hivi tunatoa fedha kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha katika maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa ridhaa yako unipe nafasi tu kidogo niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara imeweka mikakati, mbali na mpango wa matumizi ya ardhi katika maeneo ya vijiji, sasa tunakwenda kufanya zoezi la urasimishaji kwa nchi nzima. Zoezi hili litafanyika kwa nchi nzima bila kuacha mtaa wowote, tukisaidiana na wenzetu wa benki ambao watakwenda kutoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja kuanzia kwenye kupima mpaka kumilikishwa. Mwananchi atakabidhiwa hati yake baada ya kuwa amemaliza kulipa mkopo. Mikopo siyo mikubwa kwa viwanja vya urasimishaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana tutakapokuwa tunaendelea kuhamasisha kwenye Halmashauri zetu, kwenye Wilaya zetu, tulipe kipaumbele ili tuwawezeshe wananchi wetu. Mheshimiwa Rais amesharidhia zoezi hilo lifanyike na tayari makubaliano na NMB Benki, Wizara imeshaingia nao. Tumeshaanza kama pilot area eneo la Mbarali. Kwa hiyo, tutafuata wapi, ni jitihada za Halmashauri wenyewe kuweza kuwawezesha. Ahsante.