Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Masache Njelu Kasaka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Primary Question
MHE. MASACHE N. KASAKA Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatoa matokeo ya tafiti za madini katika lugha nyepesi kwa wachimbaji wadogo ili ziwasaidie katika uchimbaji kwa kuwa Sheria ya Madini inazitaka Kampuni zinazofanya utafiti kwenye madini kuwasilisha matokeo ya tafiti hizo GST?
Supplementary Question 1
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza: Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inafanya utafiti kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo kwa maana ya PMI za wachimbaji wadogo wadogo ili ziweze kuwasaidia waachane na uchimbaji wa kubahatisha.
Mheshimiwa Spika, suala la pili hii Taasisi ya Jiolojia ina ofisi zake hapa Dodoma. Sasa je, kwa mikoa ya nyanda za juu Kusini, ina mkakati gani sasa wa kufungua ofisi kule kwa Mkoa wa Mbeya ili nasi tuweze kupata hii ofisi ili iweze kuwasaidia wachimbaji wetu wadogo? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Prof. Shukrani Elisha Manya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Njelu Kasaka Masache, Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu utafiti kwa wachimbaji wadogo, taasisi ambayo inapaswa kufanya utafiti ni taasisi yetu ya GST, lakini wao wanaweza kufanya utafiti kwa njia zile za kawaida za awali kwa maana ya jiolojia, jiofizikia na jiokemia. Ili utafiti uweze kuwa wa kufana, unahitajika kidogo uchimbaji (drilling). Sasa taasisi iliyo na vifaa vya drilling ni Shirika letu la Madini la STAMICO.
Mheshimiwa Spika, hii ni habari njema kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wengine wote kwamba wiki iliyopita taasisi yetu ya GST pamoja na STAMICO waliingia makubaliano ya ushirika ili waweze kufanya kazi Pamoja. Kwa maana aliyepewa jukumu la kutafiti, lakini hana vifaa vya drilling na mwingine aliyepewa kulea wachimbaji ana vifaa, basi washirikiane ili kwa pamoja waweze kuwa wa msaada.
Mheshimiwa Spika, sisi tunaamini kama Wizara kwamba ushirika wao huo ambao waliuingia wiki iliyopita, unakuja kuwa msaada mkubwa kwa sababu taasisi mbili chini ya Wizara zimeungana ili mmoja aweze kutafiti akiwa anatumia njia za kawaida, asaidiwe na yule ambaye ana vifaa vinavyoweza ku-drill, lakini itakuwa ni kwa gharama angalau iliyopunguzwa, siyo kama ile kwa wachimbaji wakubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na kwamba ni habari njema, wachimbaji wadogo wajue kwamba tutakapofanya drilling haitakuwa free, badala yake itakuwa kwa gharama iliyopunguzwa tukilinganisha na wale wachimbaji wakubwa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili; ni kweli kwamba GST Makao yake Makuu yapo Dodoma, lakini maelekezo ya Wizara ni kwamba kazi zake hizi zifanywe pia mikoani. Habari njema ni kwamba mwaka unaokwisha huu tulifungua ofisi Geita na lengo ni kwamba tuendelee kufungua katika kanda ili kurahisisha hasa zile kazi za maabara kwa kutumia ofisi zetu za Tume ya Madini zilizoko mikoani. Kwa hiyo, kwa kuanzia tutazitumi zile na maelekezo yetu ni kwamba shughuli zote zifikishwe kwa ofisi za RMO halafu ziletwe Dodoma na kisha waweze kuhudumiwa kwa jinsi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kadri tutakavyokuwa tunapanua shughuli na kupata watumishi wengi zaidi, tunatamani kwamba tufungue matawi kila kanda katika nchi ya Tanzania ili kurahisisha utendaji kazi wa GST.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved