Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Felister Aloyce Bura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTER A. BURA (K.n.y. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia rasilimali watu katika kukuza uchumi wa Taifa, hasa ikizingatiwa kuwa rasilimali hiyo ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa Taifa?

Supplementary Question 1

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hili na kwa kuwa vyuo vikuu vinazalisha vijana asubuhi na jioni wenye elimu nzuri ya kufanya ujasiriamali, lakini tatizo ni wapi watapata mikopo kwa njia rahisi zaidi na kwa riba nafuu zaidi? Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia hawa vijana kupata mikopo kwa urahisi na kwa riba nafuu zaidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ajira ambayo ni rahisi kwa vijana na hasa kwa wanawake pia ni kilimo; lakini kilimo kinacholimwa kwa sasa hakina tija; kwanza, masoko hayapo kwa urahisi, mazao mengine yanaoza mashambani; lakini la pili, maeneo ya kulima. Vijiji vingi havijatenga maeneo kwa ajili ya kilimo kwa vijana na hata kwa wanawake ambao wameshajiunga kwenye vikundi mbalimbali. Je, Serikali iko tayari kutenga maeneo na kuzihimiza Halmashauri zetu kutenga maeneo kwa ajili ya vijana na hata kwa wanawake ambao wako tayari kuwa wajasiriamali kupitia kilimo?

Name

Antony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na la kwanza la mikopo na mitaji kwa wahitimu wa elimu ya vyuo vikuu na elimu ya juu, ni kweli natambua kwamba vijana wengi sasa hivi wanapenda kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali hasa kilimo, lakini changamoto kubwa wanayokutana nayo ni ukosefu wa mitaji na mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeliangalia hili kwa macho mawili na katika mtazamo wa mbali kuhakikisha kwamba vijana hawa wanapata fursa ya mikopo na mitaji kwanza kabisa kupitia Mfuko wetu wa Maendeleo ya Vijana ambao umekuwa ukikopesha makundi mengi ya vijana kupitia SACCOS ambazo ziko katika Halmashauri zetu. Vilevile tumeendelea kuwa na msisitizo kwa kuwataka vijana hawa wajiunge katika makampuni na vikundi mbalimbali ili waweze kupata fursa ambazo zinatokana na mikopo na mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunayo program maalum sasa hivi kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, ambapo tuna program ya Kijana Jiajiri inahusisha young graduates, wanaandika proposals zao wanazi-submit katika baraza na baadaye wanapatiwa mikopo na mitaji. Pia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi imezungumza kuhusu kuwawezesha vijana wakae katika vikundi na makampuni kutumia fani zao na taaluma zao mbalimbali ili waweze kukopesheka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu rai kwa vijana wote wale wa vyuo vikuu na wahitimu wa elimu ya juu kutumia fursa hii ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na mikopo inayopita katika Halmashauri zetu kwa kukaa katika vikundi na makampuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, limeulizwa swali kwamba Serikali ina nia gani ya kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za kilimo? Mwaka 2014, Wizara yetu ilikutana na Wakuu wa Mikoa wote nchi nzima hapa Dodoma na likatengenezwa azimio, ambapo moja kati ya kilichoamuliwa ni kutengeneza kitu kinaitwa Youth Special Economic Zone, ni ukanda maalum ambao utakuwa unasaidia utengaji wa maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana. Mpaka sasa tayari ekari 8000 zimeshatengwa nchi nzima kwa ajili ya maeneo haya ili vijana waweze kufanya shughuli za kilimo na biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumezungumza na Waziri wa Kilimo, yako mashamba makubwa ya Serikali ambayo wanayafanyia utaratibu sasa hivi nayo tuweze kuyatenga kwa ajili ya kuwagawia vijana waweze kufanya shughuli za uzalishaji mali.

Name

Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Primary Question

MHE. FELISTER A. BURA (K.n.y. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia rasilimali watu katika kukuza uchumi wa Taifa, hasa ikizingatiwa kuwa rasilimali hiyo ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa Taifa?

Supplementary Question 2

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii adimu. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Naibu Waziri, ipo nguvu kazi nzuri sana katika nchi hii iliyotafuta ajira binafsi; vijana wa bodaboda. Hawa vijana wa bodaboda tunawatumia vizuri wakati wa uchaguzi, baada ya uchaguzi, wanapata misukosuko ya kufa mtu. Wanasumbuliwa na Polisi. Bodaboda wangu waliopo Kakonko na nchi nzima, hawa bodaboda tunawalindaje katika ajira zao hizi? Ahsante.

Name

Antony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, hata mimi nataka nikiri kwamba kundi hili ni kundi ambalo kwa kiwango kikubwa sana, asilimia kubwa tuliopo hapa tuliwatumia katika kampeni zetu na ndio wametufanya tumefika katika jengo hili. Vile vile nataka nikiri tu kwamba, bodaboda ni biashara ambayo sisi tunaamini kwa kiwango kikubwa sana kwamba inasaidia katika kutatua changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika eneo hili imefanyaje? Kwanza kabisa, Serikali kwa kushirikiana na mamlaka zile husika hasa mamlaka za Halmashauri ya Manispaa na Majiji, kwanza kabisa kutenga maeneo maalum na kuwatambua na kazi yao iheshimiwe. Pili, tuna program maalum kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya ukopeshaji wa pikipiki, hizi bodaboda ili vijana wetu hawa ambao asilimia kubwa sana wanafanya kazi kwa watu wapate fursa ya kukopa wenyewe moja kwa moja na pikipiki zile ziwe mali zao na ziwasaidie katika kuinua uchumi wao.