Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Omar Ali Omar
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Wete
Primary Question
MHE. OMAR ALI OMAR Aliuliza:- Je ni lini Serikali itatoa ajira kwa Jeshi la Polisi, hasa ikizingatiwa kuwa haijatoa ajira tangu mwaka 2015?
Supplementary Question 1
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri, kwanza naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutupa majibu ya uhakika ya kupata ajira kwa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo nina maswali mawili madogo ya nyongeza;
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, suala la ajira kwa vijana wa Jeshi la Polisi, hasa wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Serikali ina mpango gani wa kupeleka askari 150 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo ndiyo tatizo kubwa kwa sasa hivi?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni kwamba; Jeshi la Polisi linapoajiri vijana kupitia Jeshi hili kuna tatizo/ changamoto moja kubwa kabisa; vijana wengi wanaondoka kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kuomba ajira ya Jeshi la Polisi,
Je, changamoto hii wamejipangaje kuhakikisha kwamba vijana wa Mkoa wa Kaskasini Pemba ndio wale wanaohusika hasa kutokana na sifa walizonazo kajiriwa katika Jeshi la Polisi? Ahsante sana.
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimwa Omar Ali Omar kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nataka nitumie fursa hii kwanza kumpongeza kwa kuwa Mheshimiwa Omar siyo tu amekuwa mwakilishi ama Mbunge wa Jimbo la Wete, lakini pia amekuwa anafanya kazi na kuusemea mkoa wake kwa ujumla katika mambo mbalimbali yanayohusu masuala ya siasa, uchumi na mambo mengine.
Mheshimiwa Spika, kikubwa nimwambie Mheshimiwa kwamba nafasi hizi zimekuja na zitakwenda katika kila mkoa. Na zitapita katika kamati za ulinzi na usalama kama utaratibu ulivyokuwa umepangwa. Lakini kikubwa nimwambie kwamba idadi ya nafasi alizozitaja zinaweza zikaenda mahali ambapo patakuwa pana uhitaji zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuna maeneo yana uhitaji zaidi. Kwa mfano kuna maeneo yana idadi kubwa ya watu (wananchi), kwa sababu utaratibu ulivyo ni kwamba askari mmoja analinda raia kuanzia 350 mpaka 400, kwa hiyo ikiwa mahali pana watu wengi panaweza pakapelekwa idadi hiyo. Lakini pia tutaangalia na crime rate (hali ile ya vitendo na matukio ya uhalifu ya mara kwa mara) pia yatatupa sisi impetus ya kuona wapi tuangalie itakavyowezekana.
Mheshimiwa Spika, lakini kikubwa nimwambie Mheshimiwa, kwamba katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, nafasi hizi zitakwenda na vijana wataomba na Serikali itaendelea kutekeleza azma yake ya kuwaahidi wananchi na kuwatekelezea. Asiwe na wasiwasi wananchi/vijana wake wataajiriwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu changamoto ya vijana kutoka mkoa mmoja ama wilaya moja kwenda nyingine kuomba hizi nafasi. Kiutaratibu sifa inayokuja anatakiwa awe Mtanzania, haikusema kwamba atoke Pemba au Unguja au wapi. Kwa hiyo anaweza akatoka sehemu moja akaenda nyingine.
Mheshimiwa Spika, lakini kikubwa tuwaambie kwamba watakaosimamia nafasi hizi wahakikishe vijana ambao wako katika mkoa husika wapate hizi nafasi ili lengo na madhumuni vijana waweze kupatiwa ajira kama ambavyo Serikali iliwaahidi wakati wa kampeni. Nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved