Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Samweli Xaday Hhayuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hanang'
Primary Question
MHE. SAMWELI H. XADAY aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kituo cha kupooza umeme Mjini Katesh kwani kuna line ndefu ya Km 780 hivyo kusababisha umeme kukatika mara kwa mara Wilayani Hanang?
Supplementary Question 1
MHE. SAMWELI H. XADAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, la kwanza, kwa kuwa kwa sasa Serikali haina utaratibu wa kufuata mipaka ya kiutawala katika kutoa huduma za umeme, kwa mfano, Kata ya Masakta iko kwenye Wilaya ya Hanang kiutawala lakini inahudumiwa na TANESCO Babati na hii imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wananchi kufuatilia huduma. Je, Serikali ina mkakati gani kurekebisha tatizo hilo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali imefanya kazi kubwa kwenye mradi wa REA kupeleka umeme vijijini lakini kwenye vijiji husika maeneo yanayofikiwa au watu wanaopata umeme ni wachache. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wananchi wengi zaidi wanapata umeme na kufika kwenye hatua ya vitongoji hasa kwenye Jimbo langu la Hanang? (Makofi)
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Samweli Xaday, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna baadhi ya maeneo ambapo mikoa au wilaya za ki-TANESCO haziendani na mikoa au wilaya za kiserikali na nia kuu ya Shirika la TANESCO chini ya Serikali ilikuwa ni kuhakikisha kwamba huduma zinawafikia wananchi katika maeneo ambayo yanafikika kirahisi. Kwa kutoa mfano katika Mkoa wa Manyara, Wilaya ya Kiteto inahudumiwa na Mkoa wa Dodoma lakini tunayo wilaya ya ki-TANESCO inaitwa Simanjiro na wilaya nyingine inaitwa Mererani. Wilaya ya Simanjro ki- TANESCO inahudumiwa na Mkoa wa Kilimanjaro lakini wilaya ya ki-TANESCO ya Mererani inahudumiwa na Arusha.
Mheshimiwa Spika, kwa wanaofahamu ni rahisi sana kutoka Simanjiro kwenda Kilimanjaro, ni rahisi sana kutoka Mererani kwenda Arusha kuliko kurudi Makao Makuu ya Mkoa wa Manyara ambapo ni Babati.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nia ya Serikali ilikuwa ni kuhakikisha kwamba huduma zinawafikia wananchi kirahisi wanapohitaji kwenda ofisini kupata huduma lakini pale ambapo TANESCO inatakiwa iende kuwafuata wananchi kuwahudumia au kwenda kufuata vifaa katika bohari.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepiga hatua kubwa sana ya kuhakikisha miundombinu inafika karibia kila sehemu na hivyo ni rahisi sana kufikisha huduma kwa wananchi mbalimbali kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, kila inapowezekana Serikali imeamua sasa ipeleke utawala wa ki-TANESCO sawasawa na utawala wa kiserikali ili kuhakikisha mtu anapata huduma kutoka kule ambako anategemea kuipata na maendeleo hayo ataendelea kuyaona kadri muda unavyozidi kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili ni kweli na kama tunavyofahamu maendeleo ni hatua. Kwa harakaharaka tu mwaka 2007 wakati REA inaanza ilipita vijiji 506 ndio vilikuwa na umeme lakini taarifa zinaonyesha kufikia 2015 tulikuwa tuna vijiji 2018 vyenye umeme na kufikia mwaka huu 2021 taarifa zetu zinaonyesha tuna vijiji 1950 kati ya 12,268 ambavyo viko Tanzania kwa ujumla wake. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba maendeleo ya kupeleka umeme ni endelevu na kadri Serikali inavyoendelea kupata pesa kwa kujibana na kwa kujihamasisha yenyewe inaendelea kuepeleka huduma hii na tutahakikisha inamfikia kila mwananchi anayehitaji kulingana na upatikanaji wa fedha.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved