Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Michael Constantino Mwakamo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Primary Question
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Makofia kupitia Mlandizi hadi Vikumbulu Kisarawe?
Supplementary Question 1
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri juu ya ujenzi wa barabara hiyo, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imeshafanya upembuzi yakinifu wa kilometa hizo 100 ambazo zinatokea Makofia kuendelea Kisarawe, je, ni lini Serikali italipa fidia wananchi hawa ili kupisha ujenzi huo uendelee kwa sababu ni wa muda mrefu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa barabara hii; na kwenye majibu yake anakiri kwamba ametenga pesa ya kufanyia ukarabati wa muda wakati wakisubiri tukipata pesa, naomba niifahamishe Serikali kwamba kwa sasa barabara hii haijafanyiwa ukarabati huo kwa miaka mingi. Kwa kuwa pesa hizi zimepangwa mwaka huu wa bajeti, je, Serikali haioni sasa ni muda sahihi kutafuta fedha za haraka kuzifanyia ukarabati barabara hizo kwa sasa kwani kipande cha kutoka Mlandizi kwenda Mzenga kina mashimo makubwa utadhani mabwawa ya kuvulia samaki? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimwa Michael Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kila hatua inayofanyika ndiyo ujenzi wenyewe wa barabara ya lami unavyoendelea. Barabara hii haitaanza kujengwa mpaka kwanza fidia ya wananchi hawa ambao bahati nzuri tayari wameshatathminiwa watakapolipwa.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mwakamo kwamba wananchi hawa watalipwa fidia pale tu ambapo Serikali itapata fedha. Jitihada kubwa zinafanywa na Serikali kuhakikisha kwamba tunapata fedha ili tuweze kuwalipa hao wananchi ambao tayari wameshaainishwa.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili kwamba barabara hii haijafanyiwa matengenezo; naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia Bunge hili naomba kumuagiza Meneja wa Barabara Mkoa wa Pwani aweze kutembelea barabara hiyo na kuangalia upungufu uliopo aweze kuikarabati kwa sababu fedha imetengwa ili wananchi waendelee kupata huduma ya barabara hii. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved