Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Francis Leonard Mtega
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbarali
Primary Question
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza:- Je, Serikali ina mikakati gani wa kumaliza mgogoro kati ya Hifadhi ya Ruaha na Wakulima na Wafugaji wanaozunguka Hifadhi hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Moja, hivi tunavyoongea, juzi makundi makubwa ya tembo wamevamia vijiji vyote vitano vya Kata ya Igava na wameshambulia mazao yote; mahindi, mpunga na maboga. Sasa wananchi wale wapo hatarini kupata janga la njaa. Ni lini Serikali itawalipa fidia wale wananchi kuwanusuru wasipatwe na janga la njaa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa ng’ombe wakiingia hifadhini kwa bahati mbaya, ng’ombe mmoja huwa anatozwa shilingi 100,000/=, sasa makundi ya tembo wale wametetekeza mazao yote na nimeenda juzi nimekuta ni mashimo matupu mashambani: ni kigezo gani au ni thamani gani watalipwa wale wahanga ambao ni wafugaji na wakulima wa sehemu ile? (Makofi/Kicheko)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kuhusu fidia, tumekuwa tukifanya uthamini pale ambapo kunatokea changamoto hiyo ya tembo kuingia kwenye maeneo ya kilimo na tunapofanya uthamini tuna-compensate wananchi kulingana na uthamini ulivyofanyika.
Mheshimiwa Spika, kuna uthamini wa aina mbalimbali; kuna mwananchi kuwa amepoteza Maisha, na upande mwingine kupoteza mazao na pia wananchi kujeruhiwa. Kwa hiyo, tunalipa fidia kulingana na athari ilivyojitokeza.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu changamoto ya namna ambavyo tunatoza ng’ombe shilingi 100,000/=; kwanza naomba sana wananchi watambue kwamba sisi tupo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hifadhi hizi zinalindwa na zinatunzwa kwa ajili ya manufaa ya nchi kwa ujumla na wananchi waliopo kwenye maeneo husika.
Mheshimiwa Spika, mara nyingi kumekuwa na sintofahamu hasa kwa wafugaji kwamba wanaingiza ng’ombe zao kwenye hifadhi kwa makubaliano ya watumishi walioko kwenye maeneo husika na matokeo yake wanyama ambao wanahifadhiwa kwenye maeneo yale wanakutana na changamoto za magonjwa. Sasa Serikali inajikuta inagharamia gharama kubwa kufanya utafiti wa gonjwa lililoingia kwenye hao wanyama na kuwatibu. Kwa hiyo, tunajitahidi sana kuzuia wafugaji wasiingize mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi. Tutambue kwamba sheria ni sisi wenyewe tulizitunga, kwa hiyo, sisi ni watekelezaji wa sheria.
Mheshimiwa Spika, kiwango hiki kipo kwenye sheria, siyo kwamba sisi tumekiamua; kipo kwenye sheria ya Wanyama kwamba wananchi wanapoingiza mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi, basi tunatumia hiyo sheria kuhakikisha kwamba inatumika sawa sawa. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved