Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Eng. Ezra John Chiwelesa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Primary Question
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:- Serikali ilitoa shilingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo, lakini kiasi cha shilingi 204,000,000 kilirejeshwa baada ya kufunga mwaka Julai, 2020. (a) Je, ni lini fedha hizo zitarejeshwa ili ujenzi uendelee? (b) Gharama ya ujenzi ni shilingi 1,500,000,000; je, ni lini kiasi cha shilingi 1,000,000,000 kitatolewa ili kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na pesa ambayo tumeipata hiyo shilingi bilioni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa sababu majengo yanaelekea kukamilika na tumefikia mwisho sasa, ni nini mpango wa Serikali kutupatia vifaatiba ili majengo haya angalau yaweze kuanza kufanya kazi haraka iwezekanavyo kwenye robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2021/2022?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu hospitali hii bado ni sehemu ya kwanza itakuwa haiwezi kulaza wagonjwa, ni nini mpango wa Serikali kwenye kutupatia ambulance mpya na ya kisasa ili angalau wagonjwa wale ambao hawataweza kupata huduma kwenye Hospitali ya Wilaya waweze kukimbizwa na kupatiwa huduma sehemu nyingine kipindi tunaendelea na kukamilisha ujenzi wa awamu ya pili? Ahsante sana.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Eng. Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba majengo haya ya Hospitali ya Halmashauri ya Biharamulo yako katika hatua za mwisho za ukamilishaji. Katika mpango wa bajeti wa mwaka 2021/2022, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kwenda kununua vifaatiba kwa ajili ya hospitali hizi mpya ambazo zinaendelea na ujenzi. Kati ya hospitali hizo, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ni moja ya hospitali ambazo zitatengewa bajeti hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili tunahitaji kuwa na magari ya wagonjwa katika hospitali zetu za halmashauri na mipango ya Serikali inaendelea kufanyika ili kuona namna ambavyo tunaweza tukapata magari hayo na kuyafikisha katika halmashauri hizi. Kwa hivyo, Hospitali ya Halmashauri ya Biharamulo ni moja ya hospitali ambazo zitawekewa mpango wa kupata gari la wagonjwa ili tuweze kuboresha zaidi huduma za afya katika eneo hilo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved