Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Bupe Nelson Mwakang'ata
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini barabara ya kutoka Kilando – Katete – Kazovu – Korongwe katika Wilaya ya Nkasi itakamilika?
Supplementary Question 1
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya barabara hiyo, lakini barabara hiyo imechukua muda mrefu sana, zaidi ya miaka mitano haijatengenezwa kabisa na madaraja yote yamekatika kabisa. Wananchi wa Kata ya Isaba, Kazovu, Bumanda, Korongwe, Katete wanapata tabu sana wakati wanapotaka kwenda kupata huduma za afya katika Kata ya Kirando. Swali la kwanza; nataka kujua, ni sababu zipi zimesababisha kusimama kwa ujenzi wa barabara hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana nami mguu kwa mguu kwenda kuona tatizo lililopo katika wilaya hiyo? Ahsante. (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza tunakiri kabisa kwamba sababu kubwa ya kuchelewa ama kutokukamilika kwa wakati kwa barabara hii kwa muda mrefu ni kutokana na kuwa na bajeti finyu. Hivyo tumeendelea kufanya matengenezo ya kawaida kwa kipindi hiki cha miaka hii ambayo Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaieleza. Hata hivyo, tunaahidi mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba Serikali bado itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya barabara hii kwa ajili ya kuwasaidia wananchi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa sababu ya kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Mbunge ya kuwapigania wananchi wa maeneo ya Nkasi pamoja na Mkoa mzima wa Rukwa na najua kila siku amekuwa akitukumbushia katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye barabara hizi, nimuahidi kabisa mara baada ya Bunge hili nitaongozana naye tukawasikilize wananchi na kupatia ufumbuzi barabara hizo. (Makofi)
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini barabara ya kutoka Kilando – Katete – Kazovu – Korongwe katika Wilaya ya Nkasi itakamilika?
Supplementary Question 2
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto ya barabara ambayo imetoka kutajwa ya Kirando – Katete ni sawasawa na changamoto ya kutoka Wanging’ombe kwenye Jimbo la Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange, kutoka Wanging’ombe kuelekea Kipengele, Lupira, Kijombo hadi Lumbira ile barabara ambayo iko chini ya TARURA. Naomba kuuliza, je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa sababu hadi dakika hii ninavyozungumza wakazi wamekuwa wakilala njiani wakati wanaposafiri kutokana na changamoto ya barabara hiyo? Kwa hiyo, naomba majibu ya swali hili. (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Festo Sanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu na bahati nzuri ameainisha katika eneo ambalo Naibu Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange, jimboni kwake ndiko barabara ilikoanzia, lakini kwa sababu mimi na Mheshimiwa Mbunge pamoja na yeye mwenyewe anafahamu katika bajeti fedha ambazo tumekuwa tukitenga na tunaahidi mbele yako kwamba tutaendelea kutenga fedha kwa kadri zinavyopatikana kuhakikisha hii barabara inapitika wakati wote. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved