Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Daniel Baran Sillo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Babati Vijijini
Primary Question
MHE. SILLO D. BARAN aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Dareda – Bashnet – Dongobesh kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 1
MHE. SILLO D. BARAN Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pamoja na majibu hayo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshakamilika, je, ujenzi wa barabara hii unaweza ukaanza kwenye bajeti ijayo ya mwaka 2021/2022? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pilli, kwa kuwa barabara hii inafanana na barabara ya Magugu kwenda Mbuyu wa Ujerumani kupitia Daraja la Magara ambalo limejengwa na Serikali kwa thamani ya shilingi bilioni 13 hadi Mbulu; je, Serikali ipo tayari kuanza ujenzi wa barabara hii pia ili kuchochea maendeleo katika eneo hilo? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sillo Baran, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Dareda hadi Dongobesh yenye urefu wa kilometa 54 kwenye maeneo ya escarpment ambayo tulijua yana changamoto yameshajengwa kilometa 10. Pia tumekamilisha usanifu wa kina mwaka huu, kwa hiyo, tusubiri bajeti; siwezi nikasema sasa hivi lakini nadhani litajitokeza kwenye bajeti lakini kwa maana ya kukamilisha usanifu wa kina maana yake tuna mpango wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na hiyo tu ni hatua za kuelekea huko.
Mheshimiwa Spika, ameuliza barabara inayoanzia Mbuyu wa Mjerumani hadi Daraja la Magara. Barabara hii pia ipo kwenye mpango na itakamilika kufanyiwa usanifu wa kina Septemba mwaka huu. Kwa hiyo, tayari pia ipo kwenye mpango kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
Name
Shabani Omari Shekilindi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lushoto
Primary Question
MHE. SILLO D. BARAN aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Dareda – Bashnet – Dongobesh kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 2
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara ya kuanzia Mombo - Soni - Lushoto ni nyembamba mno na husababisha usumbufu mkubwa sana kwa watumiaji wa barabara hiyo hasa katika kipindi hiki cha mvua.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua barabara hiyo ya Mombo - Soni - Lushoto? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara ya Mombo - Lushoto ni nyembamba. Nimhakikishie Mheshimiwa Shekilindi barabara hii itakapoingia kwenye mpango wa kuikarabati upya na ujenzi mpya tutaiangalia; ndio maana kunakuwa na usanifu mpya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii itakapoingizwa kwenye mpango wa kuijenga upya itafanyiwa Design upya na itapanuliwa ili kuweza kuingia kwenye viwango vya sasa vya barabara za mita saba na nusu kama zilivyo barabara nyingine. Ahsante. (Makofi)
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SILLO D. BARAN aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Dareda – Bashnet – Dongobesh kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 3
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kama unavyojua changamoto ya barabara mikoani ni kubwa na kwa Mkoa wa Mara katika miaka zaidi ya mitatu, minne TANROADS Mkoa wa Mara imekuwa haipewi fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati wa barabara. Sasa tunauliza ni lini Serikali itapeleka fedha za kutosha TANROADS Mkoa wa Mara ili iweze kukarabati barabara zote za Majimbo 10 ya Mkoa wa Mara ikiwepo Bunda Mjini; barabara ya kutokea Sazira – Nyamswa; barabara ya kutoka Kinyambwiga kuja Rwagu kutokea Ng’ombe mpaka Manyamanyama? Ahsante. (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mgao wa fedha za TANROADS, fedha zinagawiwa sawa na hakuna upendeleo unaofanyika na Serikali kwenye barabara zake zote za Mikoa mbalimbali. Nataka tu nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna miradi kadhaa kwa kiwango cha lami ambayo mpaka sasa hivi inatekelezwa katika Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mbunge kwamba tunatoa fedha kwa usawa na hasa kwa miradi ambayo inatekelezwa na yeye ni shahidi zipo barabara za Nyamuswa, Bunda zinajengwa. Kwa hiyo, hatuwezi tukakamilisha miradi yote kwa wakati mmoja, lakini ni mpango wa Serikali kwamba barabara zote ambazo zimeainishwa kwenye Ilani na zimeahidiwa na viongozi zitajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved