Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Jasson Samson Rweikiza
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Vijijini
Primary Question
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:- Je, ni lini umeme utapelekwa katika Vijiji vya Buzi, Buguruka, Musina, Nsheshe na vingine ambavyo havijafikiwa na umeme katika Jimbo la Bukoba Vijijini?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu yanayotia matumaini kutoka Serikalini, lakini ametaja vijiji ambavyo bado havijapata umeme, kuna kimoja hakukisema ambacho kinaitwa Ruhoko. Kijiji hiki kimefungwa waya zote, kimefungwa transfoma, kimewekwa nguzo, kila kitu kimekamilika mwaka wa pili leo umeme haujawashwa kwa nini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; amesema vijiji nane kati ya vijiji 94 ambavyo vimesalia kupata umeme, lakini na vitongoji 515, kati ya vitongoji hivyo vyenye umeme ni 86 tu zaidi ya vijiji 400 havina umeme. Utaratibu ukoje kuhusu vitongoji hivyo?
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Samson Jasson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, na-declare interest kwamba mimi natoka Jimbo la Bukoba Mjini na kabla ya utumishi wa Bunge nilikuwa mtumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba. Kijiji cha Luoko nakifahamu kiko katika Kata ya Katoro na katika ufuatiliaji wetu Kijiji cha Luoko tayari kilishapelekewa umeme, lakini tulipata changamoto ya kutopata wateja wa kuwaunganishia umeme katika kijiji hicho na hivyo miundombinu ile ilikuwa haijaanza kufanya kazi.
Waheshimiwa Wabunge, watakumbuka kuna kipindi Mheshimiwa Waziri wa Nishati alisema kwamba, wale ambao atawapelekea umeme na hawatataka kuunganisha basi itabidi tutumie jitihada za ziada za kuwalazimisha kuunganisha ule umeme. Ningekuwa naweza kufanya hivyo na Kijiji cha Luoko kingekuwa kimojawapo ambapo tungewalazimisha wananchi kuunganisha umeme huo.
Mheshimiwa Spika, lakini tayari tumeshafanya sensitization na wananchi wa Luoko wako tayari kuunganishiwa umeme. Tumemuelekeza mkandarasi aliyekuwa anapeleka umeme katika kijiji hicho anaitwa Nakroi ambaye alipeleka umeme katika Awamu ya Pili ya Mzunguko wa REA na yuko tayari kupeleka umeme. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Kijiji cha Luoko kitapepekewa umeme ndani ya muda mfupi baada ya utaratibu wa kuunganishiwa wananchi kuwa umekamilika.
Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili kuhusiana na vitongoji vya Jimbo la Bukoba Vijijini; upelekaji wa umeme kwenye vitongoji ni zoezi endelevu na kama ambavyo nimekuwa nikisema, tunapeleka umeme kwenye vitongoji katika njia tatu; kwanza TANESCO wamekuwa wakiendelea kupeleka umeme katika maeneo ya vitongoji vyetu, lakini njia ya pili ni kupitia hiyo miradi ya REA ambayo tumekuwa tukipeleka umeme kwenye vijiji na tunapeleka kwenye vitongoji, lakini njia ya tatu uko mradi maalum wa kupeleka umeme kwenye vitongoji unaoitwa densification. Na tulianza na Densification Awamu ya Kwanza tulipeleka katika mikoa nane, tukaja na Densification Two (A) tukapeleka katika mikoa tisa na sasa tuko Densification Two (B) inaendelea katika mikoa kumi na tutamalizia na Densification Two (C) ambayo tunatarajia ianze mwezi Julai kupeleka katika mikoa inayobakia.
Mheshimiwa Spika, tukiri kwamba hatuwezi kupeleka katika vitongoji vyote kwa wakati mmoja, lakini kama tunavyosema upatikanaji wa fedha na upelekaji wa umeme ni zoezi endelevu tunaamini ifikapo 2022 vijiji vyote Disemba vitakuwa vina umeme na kwenye vitongoji tutaendelea kupeleka kwa kadiri ya kuhakikisha kwamba, kila mwananchi anafikiwa na huduma ya umeme. Serikali Sikivu inapeleka umeme kw wananchi kwa maendeleo yao wenyewe.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved