Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Soud Mohammed Jumah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Donge
Primary Question
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH (K.n.y. MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Askari wapya Pamoja na kuleta vitendea kazi vya kutosha kwa Polisi Zanzibar inayokabiliwa na upungufu mkubwa wa Askari kutokana na wengi kufikia umri wa kustaafu?
Supplementary Question 1
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ningeomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa vile tokea mwaka 2012 hadi leo hii ni miaka tisa imepita na idadi ya askari polisi imeendelea kupungua kutokana na askari wengi kustaafu katika maeneo ya Zanzibar.
Vilevile kuongeza kwa vitendo vya uhalifu katika baadhi ya maeneo, je, Mheshimiwa Waziri au Serikali haioni haja ya kuajiri askari zaidi katika maeneo ya Zanzibar na hasa mashambani ili kuweza kuziba hilo pengo kwa haraka? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali namba mbili, kwa vile askari jamii katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, wamekuwa ni msaada mkubwa na tayari kuna good practices katika baadhi ya maeneo. Je, Serikali haioni haja ya kuweza kupanua wigo wa askari jamii kwa kuwapatia mafunzo na motisha, ili kuweza kufanya kazi na kuweza kusaidia kupunguza vitendo vya uhalifu katika maeneo ya Zanzibar? Ahsante. (Makofi)
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ili tuweze kufanya uajiri kuna mambo lazima tuyaangalie. La kwanza, lazima tuhakikishe kwamba, tumepata kibali cha kufanya uajiri kitu ambacho nataka nimuambie Mheshimiwa Mbunge, tumeshakifanya na tumo mbioni kuhakikisha kwamba, tunapata ruhusa ya kufanya uajiri.
Mheshimiwa Spika, lingine ili tuweze kufanya uajiri maana yake lazima tuhakikishe kwamba tuna bajeti ya kutosha kwasababu tukisha waajiri lazima tuwalipe. Sasa kikubwa ambacho nataka nitoe wito hapa leo kwa Waheshimiwa Wabunge, hasa Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza swali na Waheshimiwa Wabunge leo tukijaaliwa hapa tunaenda kupitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mheshimiwa Spika, tunaomba bajeti hii tuipitishe kwasababu, ndani ya bajeti hii imezungumzwa taarifa za ajira za vijana hasa kwenye jeshi la polisi. Kwa hiyo, nawaomba tupitishe hii bajeti ili sasa tuweze kufanya hizo harakati za uajiri.
Mheshimiwa Spika, nimeulizwa pia suala kuhusu namna bora ya kuweza kuwaboresha askari jamii. Nimuambie Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi tunavyozungumza tayari Kamishna anayeshughulika na masuala ya askari jamii na ulinzi shirikishi Zanzibar kwanza, anachokifanya ni kutoa mafunzo kwa masheha na kamati za ulinzi na usalama za shehia na vijiji, ili lengo na madhumuni ni kuona namna bora ya kuweza kuwashirikisha wananchi katika kupata ulinzi. Lakini tayari kuna mfumo mzuri, mwongozo mzuri ambao umeshatolewa umeshaanza kutumika Unguja na Pemba soon inshalah utaanza kutumika. Nakushukuru. (Makofi)
Name
Zuberi Mohamedi Kuchauka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Primary Question
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH (K.n.y. MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Askari wapya Pamoja na kuleta vitendea kazi vya kutosha kwa Polisi Zanzibar inayokabiliwa na upungufu mkubwa wa Askari kutokana na wengi kufikia umri wa kustaafu?
Supplementary Question 2
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Liwale ni Wilaya ambayo iko mbali sana na makao makuu ya Mkoa ambako ni Lindi. Na pale Liwale hakuna kituo cha polisi kwa maana ya jengo hawana kabisaa, wanaishi kwenye nyumba ambayo ilipangwa na benki mpaka leo hii. Lakini, mwenyewe ni muhanga katika hili, mwaka huu mimi nimechomewa nyumba mbili na magari matatu wakati wa uchaguzi. Kimechangiwa sana na uhaba wa askari polisi na hatuna msaada wa karibu kutoka Liwale mpaka Nachingwea ni zaidi ya kilomita 120 mpaka Lindi zaidi ya kilomita 300. Sasa, je, Serikali ina mkakati gani kwanza, kutuongezea polisi Wilaya ya Liwale ikiwepo pamoja na majengo? (Makofi)
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza niko tayari kama ambavyo umenishauri kwenda kutembea Liwale, bahati mbaya kidogo sijafika Liwale. Lakini najitahidi katika kipindi hiki cha Bunge la Bajeti tunaweza tukatenga siku moja tukaenda Liwale kwenda kuangalia hiyo hali, halafu tutarudi tuje tuone sasa namna ya kufanya tathmini kuona namna ya kuweza kusaidia.
Mheshimiwa Spika, lakini, suala hili la uhaba wa askari mimi nadhani tuje pale pale, tuhakikishe kwamba tunaipitisha bajeti yetu, bajeti ambayo imezungumza suala zima la uajiri wa polisi, vijana hawa wa polisi, ili tuweze kuajiri. Tukikwamisha hii maana yake tutakuwa hatuna namna ya kufanya. Nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved