Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Vitendo vya rushwa vimekithiri sana katika mchezo wa soka hapa nchini: - Je, ni kwa kiasi gani Serikali inakabiliana na kudhibiti hali hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali ambayo yanaonesha mwanga wa kupambana na rushwa katika michezo, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, je, ni hatua gani zimechukuliwa kwa watu ambao wamebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa katika michezo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni mkakati gani Serikali itatumia kuboresha mifumo ya uuzaji tiketi na kukusanya mapato, lakini pia kuziba mianya ili kuongeza mapato zaidi katika sekta hii ya michezo?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha kudhibiti mianya ya rushwa katika soka nchini, lakini vilevile imekuwa ikichukulia hatua watuhumiwa waliokutwa na hatia katika kujishughulisha na masuala ya rushwa. Ikumbukwe kwamba mwaka 2017 kuna watuhumiwa ambao walifikishwa mahakamani na kukutwa na hatia na hatimaye kulipishwa faini.
Mheshimiwa Spika, vilevile, mwaka 2018 kuna kesi moja ambayo ilikuwa ni maarufu sana hapa nchini, ambapo kuna mtuhumiwa alikutwa na hatia ya kula shilingi milioni 90 za Chama cha Mpira wa Miguu nchini TFF na yeye vilevile, alifunguliwa mashitaka ikiwemo ya uhujumu uchumi, lakini na baadaye kuweza kulipa fedha hizo kuzirudisha katika TFF. Kwa hiyo, tutaendelea kushughulika na watuhumiwa wa aina hii.
Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la pili la Mheshimiwa Shangazi, ili kuziba mianya sote tunafahamu kwamba sasa tunaenda kwenye ulimwengu wa teknolojia, hivyo basi, niwaase wenzetu wa TFF na timu za mipira za miguu kwamba sasa waende katika kuachana na tiketi zile za vitini vya kuchana na waweze kwenda kwenye electronic ticket, hii itasaidia sana upungufu na upotevu wa mapato, itaongeza mapato kwa timu zao, lakini vilevile kwa TFF.
Mheshimiwa Spika, vilevile niwaagize kwasababu e-government (eGA) ipo chini ya Ofisi yetu niwaagize hapa mbele ya Bunge lako Tukufu washirikiane na wenzetu wa TFF ili kuweka mfumo bora wa kukata tiketi za kuingia katika michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema katika hii trend tulioiona mwaka 2019 ya mwezi Januari kupata shilingi milioni 122 na mwezi Machi, mechi zote hizi zilikuwa ni za timu ya mpira ya Simba; kwa hiyo, kumeonekana kukiwa na timu ya Simba inacheza uwanja unajaa sana, lakini bado mapato yanakuwa hafifu, ukilinganisha na timu nyingine ambayo ni kubwa Afrika Mashariki na Kati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Name
Tarimba Gulam Abbas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Vitendo vya rushwa vimekithiri sana katika mchezo wa soka hapa nchini: - Je, ni kwa kiasi gani Serikali inakabiliana na kudhibiti hali hiyo?
Supplementary Question 2
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza na hili linahusu rushwa. Weekend iliyopita timu ya Prisons ilicheza na mabigwa wa kihistoria Young Africans kule Katavi na katika mchezo ule baada ya kumalizika na mabigwa hawa kupata ushindi kiongozi wa Prisons alisimama na kusema kwamba na amenukuliwa katika vyombo vya habari kwamba timu yake ilikua iko katika kuhongwa shilingi milioni 40 ili iweze kuachia mchezo ule.
Je, Serikali haioni sasa kwamba taarifa kama hizi ndizo za kuanzia kufanya kazi na kuwahoji watu kama hawa ili tuweze kupata ukweli? Ahsante.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tabia ya viongozi wa timu mbalimbali hapa nchini hasa wanapofungwa na Young Africans kwa halali kabisa, kutoa kauli za kwamba waliogwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ifike wakati sasa viongozi wa timu hizi na timu hizi na Watanzania kwa ujumla kwamba wakubali kwamba Young Africans, Yanga moja ndiyo timu bigwa hapa Tanzania na tibu bora hapa Afrika, kwa hiyo, wanapofungwa wakubaliane na matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Deo Ndejembi kwa kujibu maswali vizuri, hongera sana.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Waheshimiwa Wabunge, ningependa kuwahakikishia kwamba Serikali kupitia Wizara ya Michezo ninayoiongoza tunapambana na rushwa kwenye michezo kwa nguvu zote na tunashirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalaam kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi ya michezo nchini kukua bila kuwepo na mazingira ya rushwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningependa kuwapa uhakika Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania kwamba Serikali hii haitafumbia macho timu au mshirika yoyote katika michezo ambaye anatumia rushwa ili kuweza kujipatia ushindi ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved