Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jesca Jonathani Msambatavangu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Primary Question
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itarekebisha tatizo la Hospitali ya Frelimo ambayo inapata mgao kama Kituo cha Afya wakati ni Hospitali ya Wilaya ya Iringa tangu mwaka 2013?
Supplementary Question 1
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa ajili ya majibu mazuri ya Serikali, lakini naamini Naibu Waziri yeye mwenyewe ameona namna ambavyo changamoto ni kubwa. Hii ni Hospitali ya Wilaya yenye takriban wakazi 200,000 na kwa mwaka mzima wa fedha tumepewa shilingi milioni 53. Kwa hiyo, anaweza akaona ukubwa wa tatizo ulivyo na kwamba haiwezi kututosheleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, swali langu la nyongeza sasa: Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kutujengea vituo vingine vya Afya katika Jimbo la Iringa Mjini, hasa katika Kata za Kitwilu, Igumbilo, Nduli, Isakalilo na Mkwawa ili angalau kupunguza mzigo katika Hospitali ya Frelimo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, ni lini Serikali itaufanyia kazi mpango au ombi letu tulilolileta kama mkoa la kuomba sasa hospitali hizi zibadilishane maeneo; pale ilipo hospitali ya wilaya ijengwe ya mkoa na ile ya mkoa tuachiwe wilaya kutokana na eneo finyu lililopo katika hospitali yetu ya wilaya ili kufanya utanuzi zaidi kwenye eneo la hospitali ya mkoa? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Hospitali hii ya Frelimo ni hospitali ya Manispaa ya Iringa na kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu langu la msingi, hospitali hii bado ina upungufu mkubwa wa miundombinu kwa maana ya wodi kwa ajili ya kulaza wagonjwa; wodi ya wanaume, wodi ya watoto lakini pia wodi ya akinamama. Hii imepelekea pamoja na umuhimu wa hospitali hii kuhudumia wagonjwa wachache zaidi ikilinganishwa na hadhi ya hospitali yenyewe. Nndiyo maana kwa vigezo vile vya mgao wa fedha za ruzuku, inapata fedha kiasi hicho ambacho kimsingi lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatenga fedha kwa ajili ya kuongeza wodi katika hospitali ile ili ihudumie wananchi wengi zaidi na mgao wa fedha uweze kuongezeka Zaidi. Katika mwaka ujao wa fedha tumetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunajenga wodi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na ombi la kujenga vituo vya afya katika kata hizi za Kitwiru, Igumbiru, Mkwawa na nyingine nilizozitaja, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi ni kujenga vituo vya afya katika kila kata na nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge amekuwa mstari wa mbele sana kuhamasisha wananchi kujitolea nguvu zao kuanza ujenzi wa vituo hivi na sisi kama Serikali tutaendelea kumuunga mkono kuhakikisha tunatenga fedha katika bajeti zijazo kuunga mkono nguvu za wananchi katika kujenga vituo vya afya katika kata hizi kwa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni kweli kwamba Mkoa wa Iringa umewasilisha mapendekezo kwa kufuata taratibu zote kuomba Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa iweze kubadilishana na hospitali ya rufaa ya mkoa. Sisi kama Serikali tumepokea mapendekezo hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutayafanyia kazi na tathmini maombi hayo. Baada ya hapo tutatoa maamuzi ya Serikali ili kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu ya huduma za afya katika Mkoa wa Iringa.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved