Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jonas William Mbunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Primary Question
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Mbinga?
Supplementary Question 1
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, Mji wa Mbinga unakua kwa kasi na kipindi cha mvua barabara nyingi ambazo zimejengwa kwa kiwango cha changarawe huwa zinaharibika. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuongeza kiasi kilichotengwa katika msimu wa 2020/2021 na 2021/2022 ili kuhakikisha kwamba angalau kipande kirefu kijengwe ili kukidhi matakwa ya wananchi wa Jimbo la Mbinga Mjini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Serikali imefanya vizuri sana katika program ya ULGSP na TSCP na kuna uwezekano mradi wa TACTIC, je, Halmashauri ya Mbinga Mjini itakuwepo katika programu hii ya TACTIC?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipate majibu ya Serikali. (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaomba tu kwamba katika bajeti ya mwaka 2021/ 2022 Serikali iweze kuongeza fedha katika Mji wa Mbinga Mjini ili angalau Serikali iendelee kujenga barabara nyingi za kutosha. Kwa sababu bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilishapitishwa na kiwango tulichokitenga kwa ajili ya fedha kipo kulingana na ukomo, lakini katika majibu yetu ya msingi tumeainisha hapo kwamba kwa kadri fedha zitakavyoendelea kupatikana, udharura na kadhalika, tutaendelea kupeleka fedha katika Halmashauri ya Mji Mbinga ili wananchi wake waweze kupata barabara nzuri na zinazopitika wakati wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ameuliza kama Mji wa Mbinga upo katika ule mradi wa TACTIC. Nimwambie tu kabisa kwamba katika ule mradi, Halmashauri ya Mji Mbinga ipo. Ni sehemu ya ile miji 45 ambayo imeainishwa.
Name
Aida Joseph Khenani
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Mbinga?
Supplementary Question 2
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, anasema wataendelea kujenga barabara kadri wanavyopata fedha, lakini kuna maeneo ambayo yana changamoto kubwa. Napenda kujua, kuna maeneo ambayo hayapitiki kabisa ikiwemo kule kwangu Nkasi, Barabara ya Kasu – Itindi ambayo mpaka sasa wanawake wanajifungulia njiani kutokana na uharibifu wa barabara :-
Je, ni lini Serikali itakuwa na kipaumbele kwa maeneo ambayo yana changamoto kubwa?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge amejaribu hapa kuainisha kwamba tutaendelea kujenga kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Katika yale maeneo ambayo kuna shida kubwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI (TARURA) tuna fungu la dharura kwa ajili ya kurekebisha maeneo korofi kama hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, endapo patakuwa na shida basi tumekuwa tukipeleka timu ya wataalam kufanya tathmini na baada ya hapo tumekuwa tukitoa fedha kama ambavyo tunaendelea katika maeneo mbalimbali nchini hivi sasa. Kwa hiyo, katika hilo eneo ambalo ameliainisha, naiagiza Ofisi ya Raisi, TAMISEMI (TARURA) kwamba waende wakafanye tathmini halafu baada ya tathmini wailete kwetu tuone namna gani tunaweza tukasaidia wananchi wa Jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Name
Samweli Xaday Hhayuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hanang'
Primary Question
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Mbinga?
Supplementary Question 3
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Changamoto ya barabara iliyopo Mbinga ni sawa sawa na changamoto iliyopo kwenye Jimbo langu la Hanang hasa Mji wa Katesh. Ule ni Mji ambao una umri zaidi ya miaka 30 na kitu ukiwa ni Makao Makuu ya Wilaya lakini hakuna kilometa hata moja ya lami :-
Je, Wilaya ina mpango gani angalau kuweka kilometa 10 za lami ambayo pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuainisha hapa barabara ambazo ni ahadi za viongozi na sasa hivi nikuhakikishie tu kwamba Serikali ipo katika Mpango wa Kukusanya ahadi zote na kuziweka pamoja, kuzifanyia tathmini pamoja na kuzitengea bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hicho ambacho amekieleza katika Mji wa Katesh ambapo mahitaji yao yapo, nimhakikishie kuwa ahadi zote za viongozi tutaziainisha, tutazitenga katika bajeti kwa ajili ya utekelezaji ikiwemo katika mji wake wa Katesh.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved