Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Primary Question

MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi pamoja na mali zao wanakuwa salama kwani wanyamapori wamekuwa wakiingia na kufanya uharibifu kwenye vijiji?

Supplementary Question 1

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, dhumuni la eneo kinga (buffer zone) siyo kuzuia wanyama kuingia vijijini. Ni kwa jinsi gani Serikali imejipanga kuangalia usalama wa wananchi kwa sababu tembo hawa wanaingia katikati ya vijiji kule Kilangali, Tindiga, Malolo hata Yogo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ikumbukwe tarehe 15 Januari 2019 Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa Wizara saba kukaa chini na kupitia upya mipaka na kuangalia usalama wa watu katika vijiji vinavyopakana na hifadhi. Hata hivyo, mpaka sasa hatujasikia ni vijiji gani vimeshughulikiwa zaidi ya kuona wananchi wakinyanyasika na pia hakuna alama za kudumu ambazo zimewekwa kwenye eneo la kinga (buffer zone) katika vijiji vinavyopakana na mpaka.

Ni lini Serikali inaenda kuweka alama lakini pia inaenda kuanzisha game ranger post pamoja na kuanzisha vikundi vya kuzuia wanyama waharibifu katika vijiji vyetu? Nashukuru.

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpe pongezi Mheshimiwa Mbunge Dennis Londo kwa kuendelea kutoa rai kwa Serikali jinsi ambavyo wanyamapori hasa waharibifu na wakali wanavyoendelea kuathiri wananchi. Hata hivyo, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ni kwamba sasa Serikali imejipanga kuandaa mkakati ambao utawawezesha hawa wananchi kutambua ni namna gani ya kukabiliana na wanyamapori hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri tumeshaanza kutoa mafunzo katika Mikoa ya Simiyu, tumeshafanya katika Wilaya ya Busega, Wilaya ya Bariadi na maeneo mengine ambayo yanazunguka mkoa huo, lakini pia awamu inayofuata tutaenda katika Mkoa wa Ruvuma, Morogoro na maeneo mengine hapa nchini. Lengo kuu ni kuhakikisha hawa wanyamapori ambao wamekuwa changamoto kwa Tanzania na kwa nchi kwa ujumla wanadhibitiwa kwa kushirikiana na wananchi ambao wanazunguka maeneo ya hifadhi.

Name

Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Primary Question

MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi pamoja na mali zao wanakuwa salama kwani wanyamapori wamekuwa wakiingia na kufanya uharibifu kwenye vijiji?

Supplementary Question 2

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, huu uharibifu unaoletwa na wanyamapori ni mkubwa sana kwa nchi nzima na vifo vinatokea karibu kila siku tunaongea humu ndani. Hivi Serikali haioni inastahili kufanya zaidi ya inavyofanya sasa ili kuokoa maisha ya wananchi wetu? (Makofi)

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WIZARA WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inatambua changamoto hii na wananchi kweli wamekuwa wakiathirika vikiwemo vifo ambavyo vinatokea. Hata hivyo, naendelea kusema kwamba changamoto ya wanyamapori wakali imekuwa kubwa na sababu kuu ni kwamba tumevamia maeneo ambayo ni mapito ya wanyama wakali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kuona haya yote, kwa sasa hivi tumejipanga kuandaa hivi vikosi kazi vya maaskari na tutagawa orodha ya watumishi wote ambao wanazunguka maeneo ya hifadhi kuhakikisha kwamba inapotokea athari yoyote au kuonekana kwa mnyama mkali yoyote basi taarifa itolewe kwa haraka ili tuweze kudhibiti hawa wanyama wakali. Kingine ni kuhakikisha kwamba tutakapokuwa tumewafundisha hawa wananchi kujua namna ya kujikinga na hawa wanyama wakali, basi tutakuwa tumeshirikiana kwa pamoja kuhakikisha kwamba maeneo yenye hifadhi yanahifadhiwa vizuri lakini na wananchi wanaendelea kujikinga na hawa wanyama wakali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwape pole sana wananchi wote ambao wamekuwa wakikutana na hii kadhia na hata Serikali siyo kwamba inapenda kuona wananchi wake wanaendelea kupata shida ya namna hii. Tunajipanga ili kuhakikisha kwamba kadhia inapungua ama kutoweka kabisa kwa sababu hata sisi imekuwa ni changamoto kubwa lakini tunajipanga kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani.