Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Tunza Issa Malapo
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaunganisha mfumo wa gesi asilia kwa ajili ya kupata nishati ya kukaangia samaki katika Soko la Feri Manispaa ya Mtwara Mikindani?
Supplementary Question 1
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, nataka kujua ni sababu zipi zinazosababisha kusuasua kwa usambazaji wa gesi kwa matumizi ya binadamu katika Mkoa wa Mtwara hususan Manispaa ya Mtwara Mikindani?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, sisi watu wa Mtwara kabla hatujapata gesi kwa matumizi yetu, gesi imepelekwa Dar es Salaam na watu wameunganishiwa majumbani. Kwa nini wameanza Dar es Salaam badala ya Mtwara ambako gesi inatoka kwa sababu na sisi pia tuna matumizi nayo? Nakushukuru. (Makofi)
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Tunza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kusema kwamba usambazaji wa gesi katika Mkoa wa Mtwara hausuisui. Tulianza kuzalisha gesi katika Mkoa wetu wa Mtwara mwaka 2015 na mpaka sasa tunatumia umeme wa gesi peke yake kwa Mkoa wa Mtwara, Lindi na mikoa mingine yote ya Kusini. Umeme wote unaotumika kule unatokana na nishati ya gesi. Mpaka kufikia mwezi Julai mwaka huu, tayari nyumba 425 zitakuwa zimeunganishwa na huduma ya gesi majumbani kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni la kufurahisha, watumiaji wakubwa sana wa gesi Tanzania wa kwanza ni TANESCO na wa pili ni kiwanda chetu cha Dangote ambacho kiko Mtwara. Kiwanda hicho kinatoa ajira kwa vijana wetu, watu wanalipa kodi na Serikali inapata manufaa makubwa sana. Kwa hiyo, ni mojawapo ya faida kubwa sana ambayo inapatikana kule. Tunazo taasisi kama nne, Magereza, VETA, shule moja ya sekondari na chuo kingine kimoja, zinatumia gesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kusema kwa kweli Serikali imejitahidi sana kuhakikisha wananchi wa Mtwara wananufaika na nishati hii. Hata hivyo, kwa sababu nishati ni kwa ajili ya Watanzania wote basi nyingine kidogo inatoka na kwenda kwingineko mpaka hapa Dodoma tutaweza kuifikisha kwa wakati. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved