Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Amina Saleh Athuman Mollel
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AMINA S. MOLLEL (K.n.y. MHE. DKT. ELLY M. MACHA) aliuliza:- Kufuatia Mpango wa Serikali wa utoaji wa elimu bure kuanzia Elimu ya Msingi hadi Sekondari na kwamba, watu wenye Ulemavu wanakabiliwa na umasikini uliokithiri na hivyo kushindwa kumudu gharama za elimu:- (a) Je, Serikali iko tayari kutoa elimu bure kwa wanafunzi wenye ulemavu kwa ngazi ya Kidato cha Tano na Sita? (b) Je, Serikali inaweza kulihakikishia Bunge hili kwamba itaweka utaratibu mzuri wa usafiri na huduma nyingine muhimu za kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kupata elimu katika shule wanazopangiwa? (c) Je, Serikali inaweza kulithibitishia Bunge hili kwamba wanafunzi wenye ulemavu wanaoingia Vyuo Vikuu watapewa kipaumbele katika kupata mikopo bila usumbufu wowote?
Supplementary Question 1
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa watu wenye ulemavu na hasa wanafunzi, wengi wao wanatoka katika familia duni na changamoto ni nyingi:-
Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kutoa nafasi ya kipekee na ya upendeleo kwa watoto hawa wenye ulemavu, wale wanaobahatika kwenda Kidato cha Tano na cha Sita ili waweze basi kusoma bure kama walivyosoma katika elimu ya Shule ya Msingi na Sekondari?
Swali la pili, pia baadhi ya wazazi, walezi na hasa katika baadhi ya jamii zetu, huwatenga na kuwaficha watoto wenye ulemavu kwa kuwaona kuwa ni mkosi na kuwakosesha haki yao ya msingi ya kupata elimu:-
Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya wazazi au walezi wenye tabia hizi wanaokosesha watoto kupata elimu kwa sababu tu ya ulemavu walionao? (Makofi)
Name
George Boniface Simbachawene
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibakwe
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba ni jukumu la jamii kwa ujumla kwa maana ya Serikali, wananchi wote na wadau, wakiwemo wazazi na walezi wa watoto na mamlaka zao za Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba watoto hawa wanapata nafasi ya kipekee ili waweze kupata elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika utaratibu wa sasa, tumeamua kufanya kazi hiyo kwa kusaidia wale wanaoanza kuanzia chekechea, Shule ya Msingi naKkidato cha Kwanza hadi cha Nne. Kwa Kidato cha Tano na cha Sita, utaratibu huu mara nyingi tunatambua huwa unafanywa chini ya Wakuu wa Wilaya ambao hushirikiana na Halmashauri katika kuwabaini wale ambao hawana uwezo na kuweka utaratibu wa kuwasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tufahamu kwamba unapozungumzia dhana ya D by D ni pamoja na kubeba majukumu kama haya ambayo hayana utaratibu wa moja kwa moja wa kimfumo wa kibajeti. Pale kwenye Halmashauri, Mkurugenzi kazi yake siyo tu kuangalia mambo ya jumla ya kila siku ambayo yanafanywa kwa maana ya Idara zile, lakini pia kwenda zaidi na kuona jukumu lla kubeba jamii yote kwa ujumla, wakiwepo hawa wenye ulemavu na watu wengine wenye mahitaji maalumu kuhakikisha kwamba na wao wanapata haki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivi, Mkurugenzi huyu anashauriwa na Baraza la Madiwani ambalo lipo kwa ajili la uwakilishi wa wananchi kama hawa. Kwa hiyo, nina hakika hili jambo limekuwa likifanykia na hawa wanafunzi wanaohitaji nafasi ya kupata elimu kwa sababu ya mahitaji maalum na wale tu wasiokuwa na uwezo hata kama siyo walemavu wamekuwa wakisaidiwa na mamlaka hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwamba kumekuwepo na tabia ya baadhi ya jamii kuwatenga watu wenye ulemavu wasipate haki zao za msingi; tulipotunga sheria mwaka 2010, katika kifungu cha 28 cha sheria ya watu wenye ulemavu, tumezungumzia juu ya haki mbalimbali, lakini pia tumeridhia itifaki mbalimbali za Kimataifa juu ya haki mbalimbali za watu wenye ulemavu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved