Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Augustine Vuma Holle
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Vijijini
Primary Question
MHE. VUMA A. HOLLE K.n.y. MHE. SYLIVIA F. SIGULA aliuliza:- Je, nini Mpango wa Serikali kuhakikisha kuwa Timu ya Taifa Stars inafanya vizuri katika Michezo ya Kimataifa?
Supplementary Question 1
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa uvumbuzi wa vipaji, lakini pia na uendelezaji wa vipaji unapaswa kuanzia ngazi ya chini kabla ya kufika kwenye National level hasa kwenye shule zetu za sekondari, vyuo na huko halmashauri kwa ujumla. Je, Serikali haioni haja kwamba inapaswa kutenga fedha za kutosha kwenye bajeti yake ili kuendeleza vipaji vya michezo mashuleni, vyuoni na huko chini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; tumesikia kwamba, Serikali imeanzisha combination za elimu ya michezo (physical education). Nataka kujua utekelezaji wa jambo hili umefikia wapi mpaka sasa? Nashukuru sana.
Name
Pauline Philipo Gekul
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge maana yeye ni mdau mkubwa wa michezo, lakini pia niwapongeze Wabunge wote pamoja na Waheshimiwa Madiwani katika halmashauri zao kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakishirikiana na Wizara hii kwa suala zima la michezo. Swali lake la kwanza alitaka kufahamu ni kwa kiasi gani Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha michezo katika ngazi za chini inapewa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni la muhimu sana. Sisi kama Wizara nimesema tangu mwaka 2019/2020 tumeanza, lakini nitoe rai sasa kwa Waheshimiwa Madiwani na Waheshimiwa Wabunge katika ngazi za halmashauri, fedha za michezo zitengwe. Kwa hali ilivyo sasa ni Madiwani na baadhi ya wadau wanahangaika na hili suala, lakini halmashauri zetu zitenge fungu chini ya Idara ya Elimu Msingi kwa ajili ya kuhakikisha michezo inadumishwa katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili alitaka kufahamu mkakati tulionao wa Wizara kuanzisha hizi combinations za michezo kwa A Level zimefikia hatua gani. naomba nimjulishe Mheshimiwa Vuma kwamba, Kamati ilishaundwa kati ya Wizara ya Elimu, Wizara ya Michezo pamoja na TAMISEMI na ipo site ikitembelea zile shule 56 za msingi na sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Kamati hiyo kuleta majibu maana yake tunaendelea na zile shule ambazo tumeshazitambua ikiwemo Shule za Kibiti, Mpwapwa na Makambako ili kuanzisha sasa hii combination na tupate network kuanzia msingi mpaka vyuo vikuu. Endapo kazi hii itakuwa imekamilika itasaidia sana kutoa mafunzo kwa vijana wetu kuhusu masuala ya michezo. Ahsante. (Makofi)
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. VUMA A. HOLLE K.n.y. MHE. SYLIVIA F. SIGULA aliuliza:- Je, nini Mpango wa Serikali kuhakikisha kuwa Timu ya Taifa Stars inafanya vizuri katika Michezo ya Kimataifa?
Supplementary Question 2
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Nafahamu nchi inatambua kwamba, tarehe 22 kutakuwa na mchezo mkubwa ambao unaweza ukabeba record ya nchi wa Simba Sports Club na Kaiza Chiefs hapa Dar es Salaam. Nataka niulize kwa sababu, mchezo huu unaenda kubeba mafanikio ya timu karibu nne endapo Simba itafuzu, Yanga na timu nyingine. Je, ni mkakati upi wa Serikali wa makusudi kuhakikisha Simba Sports Club tarehe 22 inashinda na mashabiki wanajaa uwanjani?
Name
Innocent Lugha Bashungwa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karagwe
Answer
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nikupongeze Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kuchaguliwa na kurudi kwenye Kiti chako, unatosha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi. Sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tumekuwa tukisema timu inaposhinda na kuiwakilisha nchi yetu inakuwa ni timu ya Taifa. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuipongeza Simba Sports Club kwa hatua waliyofikia na nitoe wito kwa Watanzania wote kuhakikisha tunaiunga mkono timu ya Simba Sports Club ili match itakayoicheza tarehe 22 waweze kupata ushindi. Ushindi huo utakuwa ni heshima kwa nchi yetu. Kwa hiyo, tunawatakia heri Simba Sports Club na sisi Serikali tuko pamoja nao pamoja na vilabu vyote nchini kwa manufaa ya maendeleo ya michezo nchini. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved