Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ghati Zephania Chomete
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:- Je, Serikali ina teknolojia gani mbadala ambayo itaepusha kutumia magogo kama matimba kwenye mashimo ya migodi hasa maeneo ya Nyamongo, Tarime, Buhemba na Butiama?
Supplementary Question 1
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali machache ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imesema kwenye majibu yake ya msingi kuwa teknolojia mbadala itakayotumika sasa ni ujenzi wa zege kwa kutumia nondo. Je, ni lini teknolojia hii itawafikia wachimbaji wale wadogo wa Nyamongo, Butiama, Tarime na Buhemba ili waweze kufanya uchimbaji wenye tija kwao na kwa Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali imekiri kuwa kinachopelekea kutumia miti, mitimba na magogo kwenye mashimo ni ufinyu wa mitaji waliyonayo wale wachimbaji. Je, ni lini Serikali itawawezesha kwa kuwapa mitaji wachimbaji hao ili waweze kukidhi mahitaji hayo? Ahsante. (Makofi)
Name
Prof. Shukrani Elisha Manya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena niweze kujibu maswali ya nyongeza mawili ya Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza linazungumza juu ya lini teknolojia hii itafikishwa kwa wachimbaji wadogo. Nimpe taarifa tu, Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mojawapo ya Migodi ya Wachimbaji Wadogo ya Kalende katika eneo la Tarime tayari mgodi mmojawapo wa Mara Mine umekwishaanza kutumia teknolojia hii kuashiria kwamba kumbe teknolojia imefika. Kwa sababu inahitaji kusambazwa kwa wengi nitumie nafasi hii, kumuagiza Afisa Madini Mkaazi wa Mkoa wa Mara, Ofisi yetu ya Musoma, aanzishe mafunzo kwa wachimbaji wote wa maeneo hayo ili waweze kuipokea teknolojia hii.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kuhusu uwezeshaji. Itakumbukwa hapa kwamba, mwaka jana 2020 Tume ya Madini ilianza kutoa semina kwa mabenki yetu nchini ili kujenga awareness ya kwamba, uchimbaji madini ni biashara inayolipa kama biashara nyingine. Tulipokuwa tukisoma bajeti yetu hapa, tulithibitisha jinsi ambavyo mabenki yamepokea kwamba, biashara ya madini inawezekana na ni kweli kwamba tayari mabenki yameanza kuwezesha wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutakachokifanya ni kuendelea kutoa elimu hii kwa mabenki ili kwamba, watambue maeneo ambayo yanapata tija katika uchimbaji na kwa jinsi hiyo waweze kuelekeza fedha katika kuwezesha wachimbaji wadogo. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved