Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Santiel Eric Kirumba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza:- Je, Serikali haioni umuhimu wa kuunganisha mifuko ya mikopo iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwezesha makundi maalum kupatiwa mikopo kwa urahisi zaidi?
Supplementary Question 1
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mpango wowote wa kuzigawanya fedha hizi katika Halmashauri hususan zile Halmashauri ambazo makusanyo yake yamekuwa madogo katika asilimia 10 ambazo zinatengwa. Halmashauri hizo mfano ni Wilaya yetu ya Shinyanga Vijijini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa nini Serikali isiongeze zile asilimia kutoka asilimia 10 mpaka tano kwa wanawake kutokana na wanawake wamekuwa ni watu wazuri sana katika marejesho? Ahsante. (Makofi)
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali inayo mpango wa kuweza kufanya mapitio na kuweza kuweka maboresho zaidi kwenye mifuko hii kwa sababu ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya Halmashauri nyingine zenye kipato cha chini zile asilimia nne kwa wanawake, nne kwa vijana na mbili kwa watu wenye ulemavu kwenye maeneo mengine wanapata pungufu zaidi ya hapo. Kwa hiyo, hilo nalo ni jambo ambalo tumeshalichukua kama Ofisi ya Waziri Mkuu na limekwisha kuanza kufanyiwa vikao vya tathmini na kuweza kuangalia namna gani tutaweza kuboresha ikiwa ni sambamba na ule mjumuisho wa mifuko hii inayoshabihiana.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo lingine tumeona kwamba mikopo inayotolewa kwenye Halmashauri tunajaribu kuangalia zaidi tija, vikundi vimekuwa vikijiunga kwa ajili ya lengo la kupata mikopo ile, lakini baada ya hapo vinasambaratika na hawaendi kufikia azma ya kukopea mikopo hiyo na mpaka sasa tukisema katika mifuko tu ya fedha za Halmashauri ni mabilioni mengi ambayo bado hayajaweza kufanyiwa marejesho. Na kwa Ofisi ya Waziri Mkuu peke yake tuliwahi kutoa shilingi bilioni 4.9 lakini katika fedha hizo, ni shilingi milioni 700 tu ambazo ziliweza kurudishwa, zaidi ya shilingi bilioni nne bado hazijaweza kurejeshwa.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili Mheshimiwa Santiel Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum kwamba kuona ongezeko la asilimia; hili ni eneo pia nalo ambalo tumekuwa tukilifanyia kazi kuweza kuona namna gani tunaweza tukaboresha Zaidi hasa kwa wale waliokuwa waaminifu katika kukopa kwa sababu lengo la Serikali na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni kuwawezesha wananchi hawa kiuchumi wanapokopa hizi fedha waweze kuzirudisha ili watu wengine waweze kufanyia biashara zaidi. Na tunategemea waweze ku-graduate kwenye hilo eneo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kweli tunalifanyia kazi na tunatarajia hivi karibuni hasa kwenye mwaka huu wa fedha, fedha hizi zinazotolewa tuone ile tija na hasa twende hata kwenye kukopesha vifaa kuliko fedha ambapo mara nyingi zimekuwa zinatumika vibaya. Nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved