Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mohamed Suleiman Omar
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Malindi
Primary Question
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR aliuliza:- (a) Je, ni hatua gani zilizofikiwa kwenye mapambano dhidi ya madawa ya kulevya nchini? (b) Je, ni watu wangapi wamekamatwa kuanzia mwaka 2019 – 2020 na wangapi wamehukumiwa kifungo?
Supplementary Question 1
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri, ningeomba tu niwe na swali moja tu la nyongeza kwa sababu majibu yake kwa kweli yamekamilika lakini ninalo swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nimepata malalamiko kutoka kwa wananchi wanapokwenda kutoa mashirikiano kwenye kitengo hiki cha madawa ya kulevya kwa kuwataja wanaohusika, baadhi ya maofisa hutoa taarifa zao za siri na kuwafikia wenyewe. Je, ni hatua gani mtakazozichukua endapo mtawabaini maofisa hawa ambao sio waaminifu ili wananchi warejeshe imani ya kwenda kusaidia Serikali? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Jenista Joackim Mhagama
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Peramiho
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, najua ni miongoni mwa Wabunge ambao wamekuwa mstari wa mbele kushughulikia tatizo hili la dawa za kulevya nchini na hasa kwa pande zote mbili za muungano, nakushukuru na nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya uongozi wa Mamlaka na kama mlivyoshuhudia kilogramu takribani kama 895 kwa mara ya kwanza mzigo mkubwa umekamatwa mwaka huu kwenye Pwani ya Mkoa wa Mtwara ambayo ilikuwa inatoka Mashariki ya Mbali huko kwa hiyo ninawapongeza wote na Rais wetu tunampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa tumekuwa na tatizo kubwa, baadhi ya watendaji na maafisa ndani ya Mamlaka lakini na vyombo vingine wamekuwa wakitoa siri, sio za watoa habari tu, hata siri ya mipango na mikakati ya kwenda kudhibiti na kuzuia matumizi na biashara hii na matumizi ya dawa za kulevya. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mara zote tunapowabaini tumekuwa tukichukua hatua kali na wakati mwingine kuwafungulia mashtaka na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili waweze kuondoa kabisa tatizo hilo la ufichaji wa mianya ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa onyo kwa watendaji wote wa Mamlaka na watendaji wengine wote kutokuthubutu kabisa kuwa ni sehemu ya biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya nchini kwa ustawi wa vijana wetu na Taifa letu kwa ujumla. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved