Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa ulioanza tangu Desemba, 2020 ambao umefanya gharama za maisha kupanda?
Supplementary Question 1
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba bado bei ya bidhaa sokoni ni kubwa na haijashuka hasa kwenye vifaa vya ujenzi. Je, Serikali inasema nini juu ya suala hili?
Mheshimiwa Spika, ni takribani miaka kama mitano au kumi hatujawahi kupata utulivu wa uhakika wa bei ya mafuta ya kula, sukari na unga wa ngano ambayo ni mahitaji muhimu kwa wananchi kila siku. Serikali inasema nini juu ya suala hili? (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Cecilia ni mfuatiliaji sana wa masuala haya ya mfumuko wa bei, nakumbuka hata kwenye michango yake ya hotuba mbalimbali nimewahi kujibu swali linalohusiana na mfumuko.
Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei (inflation) sio bei kama ambavyo amesema bei za bidhaa fulani bado zipo juu. Mfumuko wa bei ni ile kasi ya bei kubadilika, tofauti na bei zenyewe kama bidhaa ipo katika bei hii hauwezi ukai-judge hapa Bungeni kama ipo juu au chini kwa sababu itategemeana tu na bidhaa zenyewe zimepatikana kwa kiwango gani.
Mheshimiwa Spika, sisi tunachoongelea na tunachoshughulika nacho ni ile kasi ya bei zenyewe kubadilika na katika Tanzania utakumbuka kwa takribani karibu miaka zaidi ya 10 tumefanikiwa kushusha mfumuko wa bei na tumefanikiwa kuuweka ucheze kati ya asilimia 3.0 hadi 5.0 ambacho ni viwango vya Afrika Mashariki. Na hilo ndio lengo kubwa la kuweza kuhakikisha kwamba bei zetu hazibadilikibadiliki kwa kiwango ambacho kinasababisha vitu visitabirike katika uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili ambalo ametaja bidhaa mahususi, kuna mikakati ambayo ni mahususi kwenye mazao hayo aliyoyataja ikiwemo mafuta ya kula pamoja na masuala kama ya sukari. Utakumbuka hotuba ya Waziri wa Viwanda ilielezea vizuri jinsi Serikali ambavyo imejikita kwenye kuongeza uzalishaji wa sukari ambapo kutakuwepo na upanuzi wa mashamba pamoja na uzalishaji wa sukari ambao sasa utaenda kutoa jibu la uhakika na la kudumu kuhusu hizo bei zinazokuwa zinapandapanda na kubadilikabadilika kwenye masuala ya sukari.
Mheshimiwa Spika, na hii ilikuwa inatokea kwa sababu, kwenye masuala ya sukari kuna vipindi ambavyo viwanda vinakuwa havizalishi. Tulikuwa tunalazimika kutafuta sukari kutoka maeneo mengine kuziba pengo la aina hiyo, lakini kwa mkakati ambao umewekwa wa kuziba pengo hilo la sukari kwa uzal;ishaji wa ndani, utaenda kutoa jibu la kudumu la mabadiliko ya harakaharaka ya bei za sukari.
Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye mafuta ya chakula utaona jinsi ambavyo Waziri Mkuu kila wakati utamuona yuko katika maeneo mahususi ambayo yanashughulika na masuala ya uzalishaji, kuhamasisha uzalishaji wa mazao haya ambayo yatatupatia mafuta ya chakula, ili kupata jawabu la kudumu la upungufu wa mafuta ya chakula ambao ndio unasababisha kupanda kwa bei. Umeona jinsi anavyofanya kazi Kigoma, anavyofanya kazi Singida pamoja na maeneo mengine ambayo anashughulikia masuala ya aina hiyo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved