Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecil David Mwambe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, nini mpango wa Serikali baada ya kukamilika kwa Mradi wa Utafiti wa Madini ya Graphite Kata ya Chiwata?
Supplementary Question 1
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kutokana na kutokuanza kwa mradi huu imesababisha kukosekana kwa shughuli za CSR kama ambavyo nilisema wakati uliopita. Kwa hiyo, Mji wa Chiwata na Jimbo la Mtama kwa sababu kuna sehemu inagusa mradi huu, Jimbo la Ruangwa pamoja na Jimbo la Newala DC imesababisha kutokuwepo kwa ajira zaidi ya 1,500 za moja kwa moja na zingine za kwenye mgodi na kukosekana kwa mapato ya Serikali pamoja na Halmashauri hizo nilizozitaja kiwango cha dola milioni 62. Sasa swali langu…
SPIKA: Eehe swali!
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, Wizara hii ndiyo iliyosababisha tufike hapa, hawaoni kwamba wanafanya hujuma kwenye uchumi wa maeneo haya niliyoyataja?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na Sheria ya Madini iliyobadilishwa mwaka 2018 ndiyo hasa chanzo cha mgogoro huu na kampuni zinazotaka kuwekeza, Serikali sasa haioni haja ya kufanya mabadiliko ya sheria hii ili wawekezaji hawa waweze kuja na mitaji yao badala ya kulazimishwa kukopa kwenye benki za ndani? Ahsante. (Makofi)
Name
Prof. Shukrani Elisha Manya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama kuna maeneo ambayo yamefaidika na mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 ni pamoja na CSR na local content. Yawezekana kweli katika maeneo ambayo miradi haijaanza Waheshimiwa Wabunge wanaweza kuwa hawajaona faida ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ila Wabunge walioko katika Mkoa wa Geita katika mikoa ambayo kuna migodi mikubwa tayari watakubaliana na Serikali kwamba ndipo mahali ambapo Serikali imeweza kubainisha sheria pamoja na kanuni za CSR na kuweza kufanya bora zaidi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara mradi utakapokuwa umeanza Serikali itasimamia sheria zake pamoja na kanuni za local content na CSR ili kuona kwamba wananchi wa maeneo husika wanaweza kupata faida.
Mheshimiwa Spika, swali la pili linahusu mabadiliko ya sheria. Mabadiliko haya yalipita katika Bunge lako Tukufu na kwa mahali ambapo sheria hizi zimetekelezwa vizuri tumeona kwamba kuna tija.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aone kwamba wawekezaji wengine wameshindwa kupata mitaji na wawekezaji wake hawa ni watu wa Australia na Australia ni mahali ambapo kulikuwa kuna total lockdown ya COVID kwa hiyo kupata mitaji mahali hapo imekuwa ni shida. Hata hivyo, tunaona kwamba wengine wanaona kwamba Tanzania bado ni mahali pazuri pa kuwekeza na Serikali kwa kweli milango ya Wizara iko wazi kuendelea kujadiliana ili tuone kwamba wawekezaji wanakuja, wanachimba na kama ilivyo sera ya Serikali wao na sisi tuweze kupata. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, nini mpango wa Serikali baada ya kukamilika kwa Mradi wa Utafiti wa Madini ya Graphite Kata ya Chiwata?
Supplementary Question 2
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo mazuri ya Serikali ikumbukwe kwamba maeneo haya yalichukuliwa karibu miaka sita iliyopita kwa upande wa Jimbo la Mtama, ikafanyika tathmini wananchi hawakulipwa fidia kwa hiyo maisha yao yamesimama kwa miaka sita. Huu mchakato umeendelea unakwenda unarudi na wananchi hawajui wafanye nini. Serikali iko tayari kutoa fidia pamoja na ile ambayo ilifanyika lakini fidia hii ya miaka sita ambapo maisha ya wananchi hawa yamesimama hawaendelei na maisha yao ya kawaida wakisubiri fidia kwa miaka sita? Serikali iko tayari sasa kutafuta namna ya kuwafidia au vinginevyo tufute wananchi waendelee na maisha yao.
Name
Prof. Shukrani Elisha Manya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tukubali kwamba mambo haya yalifanyika wakati wa transition ambapo Sheria ya Madini ilikuwa inabadilika. Ni kweli kwamba jambo hili lilionekana kama linaleta hofu na wawekezaji walirudi nyuma. Pia sheria inatoa muda wa kwamba kama fidia imefanyika na ikapita miezi sita basi fidia hiyo inaweza kurudiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu sasa mazingira yanaboreshwa tutawaomba tena tufanye fidia upya ili wananchi hatimaye waweze kulipwa. Nadhani hilo liko katika utaratibu wa sheria na hivyo sisi tutahimiza sheria ifanye sehemu yake ili fidia iweze kurudiwa na hatimaye wananchi waweze kulipwa na mradi uweze kuanza. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved