Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:- Kituo cha Afya Msindo kilichopo Wilayani Namtumbo kinapata mgao mdogo wa dawa usiokidhi mahitaji: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza mgao wa dawa katika Kituo cha Afya Msindo?
Supplementary Question 1
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ili niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri, lakini asilimia zinatotajwa hapa za mgao wa dawa unaokwenda katika Kituo cha Afya hiki si sawa na uhalisia uliopo kwenye eneo la tukio.
Mimi nimuombe sasa Naibu Waziri baada ya Bunge hili aje katika kituo hicho cha afya ajionee uhalisia wa mgao huo wa dawa kwa sababu wananchi bado wanahangaika. (Makofi)
(b) Mheshimiwa Spika, katika kituo hicho cha afya wananchi wamejitolea kujenga jengo la upasuaji kwa gharama zao wao wenyewe na kwamba wamekwama katika masuala ya vifaa vya madukani; bati, boriti, nondo, rangi na mambo mengine yanayohusiana na vifaa vya dukani. Kwa misingi hiyo, je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia katika kituo hiki cha afya ili kuweza kuwawezesha wananchi hawa waweze kupata Kituo cha Afya na nguvu zao zisipotee bure? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana; naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetangulia kujibu katika swali la msingi kwamba Serikali imeweka utaratibu uko wazi kwamba zahanati inapopandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya maombi ya Halmashauri husika yanapelekwa kwa Katibu Mkuu Afya ili kupata mgao wa dawa kwa ngazi ya kituo cha afya na si zahanati kama ilivyokuwa mwanzo.
Kwa hiyo, naomba kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Jacqueline Msongozi Ngonyani kwa kazi kubwa anayofanya kufuatilia huduma za afya katika kituo hiki cha afya, lakini nimhakikishie kwamba tumeshaelekeza Halmashauri ilete maombi hayo na tutahakikisha sasa mgao wa dawa unaendana na kituo cha afya ili wananchi wasipate changamoto ya upungufu wa baadhi ya dawa.
Mheshimiwa Spika, pili nipongeze sana wananchi wa Namtumbo na katika eneo hili la Msindo kwa kuchangia maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya na kuanza ujenzi wa jengo la mama na mtoto, lakini pia jengo la upasuaji. Nimhakikishie kwamba tutahakikisha na sisi kama Serikali tunakwenda kufanya tathmini na kutafuta fedha kuunga mkono nguvu za wananchi ili Kituo cha Afya kiweze kufanya kazi vizuri zaidi, ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved