Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Yahya Ally Mhata
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:- Je, wananchi wa Jimbo la Nanyumbu watanufaika vipi na Shamba la Uzalishaji Mifugo Nangaramo?
Supplementary Question 1
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, shamba hili la Nangaramo lilianzishwa mwaka 1986 wakati Wilaya ya Nanyumbu ikiwa chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Ukubwa wa shamba hili ni hekta 5,633; hivi ninavyozungumza kuna ng’ombe 300 tu; vijiji vinavyozunguka shamba hili vina uhaba mkubwa wa mahali pa kulima; vijiji vya Kata ya Kamundi, Mkolamwana, Kamundi na Chekereni vina shida kubwa ya mahali pa kulima hata Kata ya Nangomba, Vijiji vya Nangomba na Mji Mwema vina shida kubwa ya mahali pa kulima.
Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri; je, haoni wakati muafaka umefika maeneo haya ambayo hayatumiki kwa shughuli za mifugo wakaruhusiwa wananchi wanaozunguka vijiji hivi wakalima mazao ya muda mfupi, pale ambapo mtakapokuwa tayari basi mnaweza mkayachukua maeneo yenu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; mwaka 2018 kulikuwa na mgogoro mkubwa kati ya wanakijiji cha Mkolomwana na shamba hili, hali iliyopelekea kijana mmoja kupoteza maisha Bwana Ahmad Swalehe na vijana 36 kupelekwa mahakamani. Kwa kuwa kesi ile imekwisha na vijana wale wameachiwa huru kutokuwa na hatia katika mgogoro huu; nini hatma ya kijana huyu marehemu ambaye amepoteza maisha yake kwenye mgogoro huu, je, Serikali ipo tayari kumlipa fidia? (Makofi)
Name
Abdallah Hamis Ulega
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahya Mhata kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, namuelewa Mheshimiwa Mhata na juu ya jambo la mahitaji ya wananchi wa kata na vijiji alivyovitaja vinavyozunguka shamba letu la Nangaramo. Naomba nichukue jambo hili kwa niaba ya Wizara, tutakutana na Mheshimiwa Mhata na tuweze kukubaliana kwenda katika eneo hili la Nangaramo na kuhakikisha tunakwenda kufanya tathmini ya kuona hiki anachokisema na kuzungumza na wananchi na pale itakapoonekana inafaa tunaweza tukaona namna ya kuweza kuwasaidia wananchi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni hili linalohusu marehemu huyu; jambo hili ni kubwa, naomba nilichukue, atueleze vyema na sisi tutafanya mashauriano ya kuona namna iliyo bora ya kuweza kulimaliza suala hili, ahsante sana. (Makofi)
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:- Je, wananchi wa Jimbo la Nanyumbu watanufaika vipi na Shamba la Uzalishaji Mifugo Nangaramo?
Supplementary Question 2
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; Wilaya ya Maswa nayo ina ranchi kubwa takribani ekari 12,000 Ranchi ya Shishiu pale Maswa na Mheshimiwa Waziri analifahamu hilo.
Je, wana mpango gani wa kuwagawia wananchi wa Maswa watumie ranchi hiyo kwa ajili ya matumizi ya ufugaji maana hatuoni Serikali inafanya juhudi gani katika ranchi hiyo? (Makofi)
Name
Mashimba Mashauri Ndaki
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Magharibi
Answer
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Ulega, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa majibu yake mazuri kwa Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mawazo ya wananchi kuona kwamba maeneo ya Wizara ya Mifugo ambayo ni pamoja na ranchi na eneo ambalo analizungumza Mheshimiwa Nyongo lenyewe sio ranchi Ni holding ground, kwamba linapokuwa hivyo basi wananchi wapewe au wafanye shughuli zinginezo. Tunakubaliana kwamba tunafanya tathmini ya maeneo yote tuliyonayo ili tuone ni kwa namna gani yanaweza yakatumiwa vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa eneo la Shishiu, Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wameleta andiko na mpango wao kuonesha ni kwa namna gani wanataka kutumia hilo eneo. Wameeleza wanataka eneo dogo, sisi tumewarudishia tukawaambia leteni mpango wa kutumia eneo lote la Shishiu kwa ujumla wake halafu tutaona ni kwa namna gani sasa mnakwenda kulitumia halafu tuweze kuwapa nafasi ya kulitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe tu Waheshimiwa Wabunge na wananchi maeneo ya Wizara ya Mifugo ambayo yapo wazi, tunataka tuyatumie kikamilifu kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe, lakini sekta binafsi ili iweze kuwekeza vizuri kwenye hayo maeneo na yaweze kutumika kwa tija zaidi, ahsante. (Makofi)
Name
Agnes Elias Hokororo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:- Je, wananchi wa Jimbo la Nanyumbu watanufaika vipi na Shamba la Uzalishaji Mifugo Nangaramo?
Supplementary Question 3
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa kuwa katika swali la msingi majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ilikuwa kwamba lengo la Shamba la Nangaramo ni kusambaza mitamba, lakini katika maeneo mengi yenye mashamba haya mitamba hiyo imekuwa ndama wake wanauzwa kwa shilingi 1,500,000 na hivyo wananchi kushindwa kumudu gharama za kununua ndama.
Je, Serikali haioni haja ya kuondoa kabisa hayo mashamba na kwa vile lile lengo la msingi la kusambaza mitamba halijafanikiwa? (Makofi)
Name
Mashimba Mashauri Ndaki
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Magharibi
Answer
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; kuhusiana na bei ya mitamba, hiyo ni biashara; na ndama au ng’ombe wanaouziwa wananchi bei yake inajumlisha gharama za kumtunza yule ng’ombe pamoja na gharama zingine zote.
Mheshimiwa Spika, sasa huwezi kumnunua ng’ombe ambaye Mheshimiwa Mbunge anamuita ni ndama, actually ni ng’ombe kwa sababu huyo ng’ombe anaponunuliwa kwetu anakuwa yupo tayari kubeba mimba ili aweze kuzaa. Sasa sio ndama kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amemuita na pengine tutaangalia utaratibu ambao unapelekea mpaka kufikia gharama za namna hiyo, tuone kama tunaweza taratibu za gharama zikapungua tuweze kuwauzia kwa bei ambayo ni reasonable. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitangaze tu kwamba kwa Shamba la Nangaramo tayari tumewauzia wananchi walio karibu na shamba hilo mitamba 14 wameweza kununua na shamba letu kwa sababu linazalisha sio mitamba mingi sana, inatafutwa na wana order kubwa mpaka sasa hivi wanasubiria. Sasa suala la bei tutaliangalia tuone ni kwa namna gani inaweza kupungua ili wananchi waweze kununua mitamba mingi zaidi. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved